THBUB: KIFO CHA MAREHEMU NUSURA HAKIKUWA NA UHUSIANO WA AJALI


Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

TUME ya Haki za  Binadamu  na Utawala Bora (THBUB),imesema imekamilisha uchunguzi iliyouanzisha yenyewe kwa mujibu wa Kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Tume hiyo, Sura ya 391, kinachoipa uwezo wa kuanzisha uchunguzi na kubaini kuwa kifo cha Marehemu Nusura hakikuwa na uhusiano na ajali ya gari aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za usajili T454 DWV iliyomhusisha Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dk.Festo Dugange iliyotokea  Aprili 25 usiku wa kuamkia  Aprili 26, 2023 katika eneo la Iyumbu, jijini hapa.

Pia THBUB inapendekeza Jeshi la Polisi Tanzania na mamlaka nyingine zichukuwe hatua ili kuwabaini wale wote wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii.

Akizungumza Jijini Dodoma Juni 2,2023, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu
Mathew  Mwaimu  amesema 
THBUB haikuweza kuthibitisha mtu yeyote kuhusika na kifo cha Marehemu Nusura  Abdallah kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja, Mkemia Mkuu wa Serikali, na maelezo ya mengine ya mashahidi.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa
Mei10,2023, Tume hiyo ilitoa taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari ikielezea nia yake ya kufanya uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Marehemu Nusura, ambacho chanzo chake kilizua mkanganyiko, ambapo baadhi ya watu walikihusisha na ajali ya gari iliyomhusu Naibu   Waziri Dk. Dugange.

Amesema katika uchunguzi huo, THBUB ilitembelea eneo ilipotokea ajali ya gari iliyomhusisha Mhe. Dkt. Dugange; nyumbani kw Dk. Dugange, Kituo cha Polisi (Traffic) Mkoa wa Dodoma Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mwenyekiti  huyo amefafanua kuwa Tume hiyo ilitembelea Kijiji cha Mandewa, Kata ya Mandewa, Wilaya ya Singida Mjini wanakoishi wazazi wa marehemu Nusura Hassan Abdallah; Kitongoji cha Mtakuja Kijiji cha Kikonge, Wilaya ya Iramba alikozikwa Nusura; Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Hospitali ya Faraja iliyopo Himo, Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine kwa madhumuni ya kupata maelezo ya watu mbalimbali kuhusu ajali ya Naibu Waziri na mazingira ya kifo cha Nusura.


"Baada ya kupata maelezo katika maeneo yote ilikofika, THBUB imebaini usiku wa Aprili 25,2023 kuamkia 26  2023 ilitokea ajali ya gari maeneo ya Iyumbu, karibu na Njia Panda ya Shule ya Mfano, Jijini Dodoma ambapo gari iliacha njia, kugonga mti na kupinduka na baada ya kupata majeraha kutokana na ajali hiyo, Dk.Dugange alihangaika kutafuta msaada ili aweze kufikishwa hospitali kupata matibabu," ameeleza.

Ameongeza kuwa majira ya alfajiri ya  Aprili 26,2023, Dk.Dugange alipata msaada wa boda boda iliyomfikisha Hospitali ya Benjamin Mkapa Aprili 27 2023, Marehemu Nusura aliyekuwa Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dodoma alisafiri kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa basi la Manning Nice baada ya gari la Kapricon alilokuwa amepanga kusafiria kuchelewa.

Jaji Mstaafu Mwaimu amesema 
basi hilo la Manning Nice lilimfikisha Babati na baadaye kupanda gari aina ya Coaster mpaka Arusha na kumalizia safari yake hadi Moshi kwa basi la Ibra Line huku akisema Marehemu Nusura  alipokelewa na mchumba wake Juma Kundya, Mjini Moshi ambapo walifika nyumbani kwake saa tano usiku wa  Aprili 27 mwaka huu.

Ameeleza lengo la safari hiyo lilikuwa ni kuzungumzia masuala ya uchumba wao na kupanga siku ya mchumba wake kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Singida ambapo alipanga kukaa hapo hadi Mei 02, 2023 ndipo arejee Dodoma.

Mwenyekiti huyo  amefafanua kuwa mara ya mwisho Marehemu kuwasiliana na familia yake ilikuwa Aprili 26, 2023 na mara ya mwisho kuwasiliana na rafiki yake aliyekuwa akisoma naye Chuo Kikuu cha Dodoma ilikuwa  Mei 01, 2023 akiwa mzima wa afya na kwamba tarehe hiyo ya Mei 01  2023, Marehemu huyo  aliandaa chakula cha jioni ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.

Amesema baada ya kumaliza kula, Marehemu  alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu na kwamba Pamoja na hatua mbalimbali za kitabibu zilizochukuliwa na Madaktari wa Hospitali hiyo, Nusura  alifariki dunia majira ya saa 5:00 usiku wa Mei01, 2023.

"Vipimo vilivyofanywa na Hospitali hii vilionesha kuwa kifo cha Nusura kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu (diabetic ketoacidosis with hypovolemic shock and moderate anaemia) na Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya mazishi na kuuona mwili  kabla ya mazishi walithibitisha kuwa haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha," amesema.

Ameeleza kuwa Mabaki ya chakula walichokula Marehemu Nusura, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake; na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi, na baada ya kufanyiwa uchunguzi taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwemo kwa sumu.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI