Na Asha Mwakyonde,Dar es salaam
WAFANYABIASHARA 150 kutoka jimbo la Haryana India wametembelea maonesho ya 47 ya biashara ya Kimataifamaarufu kama sabasaba kwa lengo la kuangalia fursa za uwekezaji nchini baada ya kutembelea baadhi ya maeneo wamekiri parachichi kutoka Tanzania zina soko kubwa nchini India hivyo watajikita pia kwenye zao hilo.
Akizungumza kwenye siku ya India iliyofanyika kwenye viwanja vya maonesho hayo Katibu kiongozi wa wafanyabiashara wa jimbo la Haryana, Raasheka Vurdin amesema Tanzania inakuwa haraka hivyo wamejipanga kuja kuwekeza nchini.
“Tumejipanga kuja kuwekeza hasa kwenye sekta ya elimu, Kilimo, tehama na dawa,” amesema Vurdin.
Amesema mbali na kuwekeza katika sekta hizo wanatarajia pia kuwa na viwanda vya kusindika mazao ya mashambani.
Alisema parachichi kutoka Tanzania lina soko kubwa sana India hivyo katika kilimo watajikita pia kwenye zao hilo la parachichi.
Vurdin pamoja na wafanyabiashara hao kutoka Jimbo la Haryana walitembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na taasisi za serikali ikiwemo Kituo cha Uwekezaji kuweza kujua taratibu za uwekezaji, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Ameeleza kuwa ni mara yao ya kwanza kufika Tanzania na wanataka kuendelea kuboresha usafirishaji na uingizaji wa bidhaa kati ya nchi hizo mbili.
“Hii ni nafasi ya kwanza kuja Tanzania na tunataka kuboresha zaidi biashara kati ya nchi hizi mbili lakini pia tupige hatua kiteknolojia,” alisema na kuongeza tumefurahishwa na mfumo wa Tanzania wa kuwa na kituo kimoja cha kutolea huduma zote," amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade Profesa Ulingeta Mbamba alisema India ni nchi ya tatu kwa ukubwa kufanya biashara na Tanzania kwani mwaka 2021/2022 waliweza kufanya biashara ya takribani dola za Marekani bilioni tano.
“ Dunia inaendeshwa na biashara kwa hiyo tunatakiwa kutumia nafasi yoyote ya biashara inayopatikana ili kuweza kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Profesa Mbamba.
Ameongeza kuwa Tanzania haina budi kuendeleza mahusiano mazuri ya kibiashara yaliyopo kati Tanzania na India ili kila mmoja kujifunza mbinu mbalimbali za biashara.
Aidha Profesa Mbamba aliwataka Tantrade kufuatilia kwa karibu mikataba yote watakayoingia ili iingie kwenye utekelezaji wa haraka.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tantrade Latifa Khamis alisema jimbo la Haryana lina fursa nyingi hivyo watawajulisha watanzania fursa zilizopo na kuwaonesha njia.
“Tutahakikisha tunaondokana na ile tabia ya kwamba tunafanya maonesho basi lakini tunakikisha baada ya maonesho wao wanaondoka na fursa na sisi tunaondoka kwa kufanya mikataba mikubwa yenye manufaa ya nchi zetu mbili,” ameeleza Khamis.
0 Comments