MSIGWA:HAKUNA BANDARI ILIYOUZWA, SERIKALI INALINDA MASLAHI YA WATANZANIA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

SERIKALI imesema hakuna Bandari yoyote iliyouzwa hadi sasa, nchi bado haijafunga mkataba wowote wa utekelezaji wa Mradi wa Uendeshaji wa bandari baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai kupitia kampuni ya DP World.

Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 27,2023 Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa,wakati  Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC),likizungumzia utekelezaji wa majukumu na mwelekeo  wake wa mwaka wa fedha 2023/2024, amesema serikali ipo macho muda wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa kwenye sekta mbalimbali zikiwamo Madini, Kilimo, Maji, Usafirishaji wa Anga na Majini.

Msigwa ameeleza kuwa bandari haijabinafisihwa ,serikali inataka kushirikiana na sekta binafisi kuendesha bandari hiyo huku akisema mikatakaba na watakaoendesha bado haijasainiwa ambapo kwa sasa kuna makubaliano baina ya serikali hizo.


"Wataalam wapo mezani akiwamo
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC,Kaimu Abdi Mkeyenge wanaanza kupanga na kuandaa mikataba itakuaje,itakuwa ya muda gani, itagharimu shilingi ngapi na itakwenda kushirikiana na sekta binafisi sehemu gani," amesema Msigwa.

Msemaji huyo wa serikali ameongeza kuwa Wataalamu watakavyokamilisha majadiliano wataangalia maslahi yapo wapi, maoni yaliyotolewa na Watanzania yatazingatiwa, na kwamba wataalam hao watakapokamilisha  Watanzania wataambiwa.

"Watanzania wataambiwa tumekubaliana kushirikiana na Kampuni fulani, kuendesha bandari fulani au tumekubaliana na Kampuni fulani kuendesha gati fulani, tumekubaliana na Kampuni fulani kuweka mifumo hii na hii  na itakuwa kwa muda gani hadi sasa bado hayajafikia mwisho,"ameeleza.

Amesema hakuna bandari iliyobinafisishwa, kuuzwa, kuwapo sokoni, serikali inatafuta kushirikiana na wawekezaji ili kuongeza ufanisi wa bandari.

Msemaji huyo ameeleza kuwa Serikali itakapopata mwekezaji  Watanzania watajulishwa  ambapo kwa sasa bado hajapatikana.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI