TASAC: BILIONI 59.23 ZATUMIKA KUKAMILISHA MRADI WA MLVMCT


 Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

SERIKALI ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),linaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT ),ili kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri majini na uvuvi.

Mradi  wa MLVMCT unatarajiwa kukamilika mnano Disemba, 2024 na tayari Mkandarasi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi katika mradi huo. 

Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 27,2023 na waandishi wa habari  Mkurugenzi Mkuu wa TASAC,Kaimu Abdi Mkeyenge kuhusu utekelezaji wa majukumu na mwelekeo  wake wa mwaka wa fedha 2023/2024 wa Shirika hilo amesema lengo la mradi huo ni kushughulikia changamoto za usafiri majini,kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria. 

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda na kwamba umepangwa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za Mradi ni Shilingi bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani (national activities) na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda (regional activities) zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda.


"Hadi sasa, Mkandarasi ameshaanza ujenzi kwa vituo vidogo vya Mara-Musoma, Kanyala na Nansio-Ukerewe," ameeleza Mkurugenzi huyo wa TASAC.

Akizungumzia mpango mkakati wa TASAC, Mkeyenge amesema kusimamia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji kwa njia ya Maji inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization),na kushirikisha wadau katika kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria na Kanuni mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, sura 415.

"Napenda kuchukua nafasi hii kwa heshima kubwa kuishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan  kwa kuendelea kuiwezesha TASAC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT," ameeleza.


Ameongeza kuwa mikakati mingine ni kuboresha udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji nchini sambamba na kuweka ushindani ili kuhakikisha huduma za usafiri majini zinakuwa endelevu, kuimarisha Usalama na Ulinzi kwa usafiri kwa njia ya maji sambamba na Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira utokanao na usafiri wa Meli.

Mkurugenzi huyo ameeleza pia wana mikakati ya kuboresha usimamizi na uwajibikaji katika kupanga na kutumia rasilimali za Shirika ,kuimarisha uhusiano ya kitaasisi na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu majukumu ya Shirika hilo.

Amesema,kuboresha Sheria, Kanuni, na nyenzo za kiudhibiti katika sekta za usafiri majini na biashara ya meli pamoja na  kutekeleza jukumu la kuratibu maandalizi ya Amri, kutoa maoni na kuwezesha uandaaji rasimu za Kanuni na nyenzo za utendaji zitoazo mwongozo kuhusu udhibiti huduma za usafiri majini, usalama na ulinzi kwa vyombo vya usafiri majini na uchafuzi baharini kutoka katika meli.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha Bandari, mikataba na watakaoendesha bado haijasainiwa.

"Sasa hivi wataalamu wapo mezani kuzungumza kuhusu mikataba, muda na gharama hakuna Bandari iliyouzwa, wataalamu watakapokamilisha majadiliano tutaangalia maslahi yetu yako wapi na maoni yanayotolewa na Watanzania yatazingatia.

Ameongeza kuwa Serikali ipo macho wakati wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI