Na Asha Mwakyonde,Dar es salaam
WAKULIMA wakulima wadogo zaidi ya 9000 wameshasajiliwa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB),ili kufanya biashara ya zao la mkonge lengo likiwa ni kufahamika na kupata fursa mbalimbali zinapojitokeza kupitia zao hilo.
Bodi hiyo pia inatoa leseni ya kilimo cha zao hilo, leseni ya msindikaji na ya kufanyabiashara hapa nchini na nje ya nchi pamoja na ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.
Akizungumza jijini Dar es salaam Julai 09,2023 Afisa Masoko na Uhamasishaji wa TSB, David Magari katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF),maarufu Saba Saba, yenye kaulimbiu isemayo"Tanzania Mahali sahihi pa Biashara na Uwekezaji," ameeleza kuwa ili kuweza kufanya biashara au kulima mkonge unatakiwa usajiliwe na TSB.
Magari amesema wamekuja katika maonesho hayo ya sabasaba kwa lengo la kutoa elimu kwa watanzania, kutangaza fursa mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya mkonge na kuhamasisha matumizi ya bidhaa mbalimbali za mkonge.
"Zipo faida nyingi za wakulima, wafanyabiashara wa zao hili la mkonge ikiwamo kusajili ili kumfanya afahamike zaidi katika fursa zinazojitokeza,soko la mkonge kwa sasa ni zuri uuzaji unafanyika hakuna changamoto ya wakulima kukosa soko," ameeleza Magari.
Bodi hiyo imewataka wale wote wanaojihusisha na biashara ya mkonge nchini kufika katika katika ofisi za TSB ili kujisajili na kutambulika ikiwa ni takwa la kisheria kwa wafanyabiashara, wakulima wa zao hilo.
TSB ni taasisi ya serikali ambayo ina jukumu la kusimamia zao la mkonge na kufanya shughuli za utoaji wa leseni na vibali kwa wafanyabiashara wa zao hilo, kukusanya takwimu na kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuzisambaza kwa wateja wao.
0 Comments