Na Asha Mwakyonde,Mbeya
WAKULIMA wametakiwa kutumia fursa inayotolewa na serikali kupitia Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kurasimisha biashara zao kwa lengo la kuzikuza na kupata zabuni serikalini pindi zinapotangazwa.
Hayo yamesemwa leo 4 ,2023 jijini Mbeya na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano BRELA, Roida Andusamile,kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', ameeleza kuwa kiilimo ni biashara hivyo wakulima watumie fursa inayotolewa na serikali kwa kuhakikisha wanarasimisha biashara zao.
Amesema serikali ina nia njema na wananchi wake hivyo wakulima hao wanaporasimisha biashara inawawezesha kuzikuza na kutambulika zaidi.
Mkuu huyo wa kitengo amesema kuna faida nyingi za kusajili jina la biashara, kampuni, usajili wa alama za biashara na huduma, kupata leseni ya biashara kundi A na kupata leseni ya kiwanda ikiwamo kufanya biashara kwa kujiamini.
"Ushiriki wetu katika maonesho haya kunawapa wakulima, wananchi wanaotembelea banda hili huduma mbalimbali za papo kwa papo ikiwamo kusajili jina la biashara," amesema Roida.
Ameongeza kuwa pia Wakala huo unafanya usaidizi wa kusajili kwa njia wale wanaopata changamoto kupitia mtandao.
Bernard James mkazi wa Mbeya aliyefika kusajili jina la biashara katika banda hilo amesema kuwa amefurahishwa na huduma zinatolewa na BRELA ambapo tayari ameshapata cheti cha jina la biashara.
"Naamini nitakuwa huru katika kufanya biashara yangu hivyo nawashauri ambao wanafanya biashara bila kuzisajili waje wasajili kwani ukikamilisha taratibu zote unapata cheti chako kwa muda mufupi," amesema.
Naye mkazi wa Mtwara aliyepatiwa huduma hiyo Joseph Nzunda, ambaye anafanya Utafiti wa zao la ufuta kwa kuuongezea thamani ya ufuta huo amesema awali alikuwa hajasajili jina la biashara hivyo amepata msukumo wa kuzisajili ili awe salama kibiashara.
0 Comments