KCBL YAPONGEZWA KUONGEZA MTAJI

Na Asha Mwakyonde, Mbeya

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya ameipongeza Benki ya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KCBL),kwa
kuongeza mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 4 katika kipindi cha miaka miwili na kufikia Sh bilioni 6.

Pia ameutaka uongozi wa benki hiyo kuongeza wigo wa kufungua matawi zaidi mikoani ili kuwarahisishia wananchi huduma.

Kusaya ameyasema hayo  jijini Mbeya leo 4, 2023  wakati alipotembelea Kijiji cha ushirika kinahoratibiwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula',amesema  kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya ushirika kupitia benki hiyo.

Amesema wanaushirika wakijiunga  wengi watawezesha mtaji wa benki hiyo kuongezeka haraka  zaidi na kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

"Benki hii ili iweze kukua zaidi inategemea wanaushirika hivyo jitokezeniwana ushirika popote walipo nchini," ameeleza Katibu Tawala huyo.


Naye Mkuu wa Kitengo cha Mikopo na Biashara KCBL, Frank Wilson,
 amesema wana malengo ya kufikisha mtaji wa Sh bilioni 15 ifikapo Oktoba mwaka huu  ili waweze kupata leseni ya kuwa benki ya taifa ya ushirika. 

"Mwitikio wa watu kujiunga na benki hii ni mkubwa hali inayosababisha kuongeza mtaji wa zaidi ya Sh bilioni 4 kwa miaka miwili," ameeleza.

Ameongeza kuwa katika mwaka 2022/23 benki hiyo imekopesha zaidi ya Sh bilioni 3 na kati ya hizo Sh bilioni 1 walikopeshwa vijana na wanawake wanaojihusisha na kilimo.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA