CPB IMENUNUA TANI 35,000 ZA NAFAKA KUTOKA KWA WAKULIMA NCHINI

Na Asha Mwakyonde, Mbeya 

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko nchini (CPB), imenunu tani 35,000 za mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mpunga, alizeti na maharage kutoka kwa wakulima.

Akizungumza Agosti 7, 2023 na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, John Maige, ameeleza kazi ya kubwa  Bodi hiyo ni kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuyaongezea thamani.

Maige ameongeza kuwa  kwenye bodi hiyo kuna fursa mbalimbali zikiwemo za kuuza mazao, uwakala wa kuuza mazao na bidhaa.

Amebainisha kuwa  Bodi hiyo inaendelea na ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima katika vituo vyao vilivyopo Iringa, Arusha, Dodoma, Songea, Sumbawanga na Tunduma.


"Mwaka huu tuliweka malengo ya kutumia Sh bilioni 100 za kukunua mazao lakini hadi sasa tumetumia Sh bilioni 29," na tunazalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi amesema Maige.

"Kama kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu inavyosema tunaamini vijana na wanawake watanufaika na uwepo wa Bodi hii katika maonesho haya na baada ya Nanenane katika ofisi zetu zilizopo katika kanda mbalimbali,” amesema.

Akizungumzia mwelekeo wa CPB ameeleza ni kujiimarisha zaidi katika ufanyaji biashara kwa maana ya ununuzi wa mazao ya wakulima, kuyaongezea thamani na kuyauza katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema bidhaa wanazozalisha ni bora kwa sababu wanazingatia viwango vya ubora vya Afrika Mashariki na kimataifa kutokana na teknolojia wanazotumia.

“Tuna mitambo ya kisasa inayosindika bidhaa za unga wa mahindi, ngano na mchele. Bidhaa tunazozalisha ni bora kwa watumiaji na zinalinda afya ya walaji,” amesema Maige.


Naye Mkurugenzi wa bodi hiyo, Nicomed Bohay, amesema wanatatua changamoto za masoko ya ndani kwa wakulima. 

“Tunanunua nafaka mbalimbali nchi nzima kwahiyo tunatatua changamoto ya soko kwa wakulima wa mahindi, alizeti, mpunga, ngano na nafaka zingine.

“Baada ya kununua tunachakata katika viwanda vyetu vya kisasa vilivyopo maeneo mbalimbali ya nchi na kuuza bidhaa katika maduka ya jumla na rejareja…tunatatua changamoto ya wajasiriamali kupata bidhaa bora,” amesema Bohay. 

Bodi hiyo ina ofisi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Iringa), Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Arusha), Kati (Dodoma) na Mashariki (Dar es Salaam).

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA