ZAO LA MKONGE LAONGEZA MAUZO NJE YA NCHI


Na Asha Mwakyonde, Mbeya

ZAO la mkonge limefanya vizuri zaidi soko la nje kwa mauzo kutoka Dola za Marekani milioni 42 hadi kufikia Dola milioni 56 kwa kipindi cha miaka miwili.

Akizungumza  jijini Mbeya Agosti 7, 2023 Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saad Kambona, kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', amesema mapato ya Serikali yameongezeka tangu ilipochukua jitihada za kulifufua zao hili mwaka 2019 na kulifanya kuwa la kimkakati.

Mkurugenzi huyu amesema Soko la nje limefanya vizuri zaidi kwa sababu mkonge mwingi umeuzwa nje kuliko ndani ambapo mauzo   ya nchini yameongezeka kutoka Sh bilioni 41 hadi kufikia Sh bilioni 43.

Akizungumzia uzalishaji wa mkonge umeongezeka kutoka tani 36,000 (2020) hadi kufikia tani 48,000 (2022) na malengo ya mwaka huu ni kufikia tani 60,000.

Kambona ameongeza kuwa hadi kufikia Juni 2023 tayari wamezalisha tani 34,000 na kwamba matarajio ya Bodi ni kufikia mwisho wa mwaka huu kuzalisha tani 60,000.

"Zao hili lina fursa na linastahimili ukame linaweza kubadilisha hali za maisha ya Watanzania kwa muda mfupi na wastani wa bei ya nyuzi za mkonge kwa tani moja kwa sasa ni Sh milioni 3.5," ameeleza Kambona.
 
Ameongeza kuongezwa kwa bajeti ya maendeleo ya bodi hiyo kutoka Sh milioni 100 mpaka kufikia Sh bilioni 2 kwa mwaka ni kutoka na jitihada kubwa zilizofanyika.

"Hatua hii imeiwezesha bodi kupata vitendea kazi yakiwemo magari yanayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa takwimu, kuboresha mitambo, kugawa mbegu bure na ugawaji mashamba kwa wakulima wadogo ambayo yalitaifishwa na Serikali wilayani Kilosa," amesema.


Naye Mtendaji Mkuu wa Kampuni tanzu ya NSSF inayojihusisha na uongezaji thamani zao la mkonge, Elizabeth Kalambo, amesema
 kampuni hiyo ina wafanyakazi 1008.

Amesema uwepo kwa kamba za plastiki ni changamoto kwa Kampuni hiyo ya soko la uhakika la bidhaa za mkonge.

Post a Comment

0 Comments

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA MIFUMO THABITI YA NISHATI JADIDIFU KUKIDHI MAHITAJI YA NISHATI