Na Asha mwakyonde, Mbeya
WAKULIMA wa mazao mbalimbali yakiwamo mahindi, mpunga na viazi, wameushukuru Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), kwa kuwapatia elimu ya namna wanavyoweza kulima kilimo chenye tija.
SAGCOT ni Mpango wa Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi uliozinduliwa wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani Africa (World Economic Forum Africa) uliofanyika Dar-es-Salaam mwaka 2010 ambapo Utekelezaji wake unachukua kipindi cha miaka 20 hadi mwaka 2030 lengo kuu likiwa ni kuongeza tija ya uzalishaji kwenye kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza umaskini na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa mazingira kupitia urasimishaji wa kibiashara kwa wakulima wadogo.
Wakizungumza jijini Mbeya leo Agosti 7, 2023, katika banda ambalo limeratibiwa na SAGCOT wakulima kutoka mikoa ya Mbeya na Njombe Atufena Mbembati
na Neema Mgaya kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula'.
Wakulima hao wamesema kuwa SAGCOT imekuwa ikiwasaidia katika mambo mbalimbali yakiwamo kuwapelekwa kwenye mafunzo yanayolenga kuongeza tija kwenye mazao yao.
Atufena ni mkulima wa mpunga kutoka Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya amesema kuwa kilimo hicho alianza tangu mwaka 1997 akiwa analima hekta moja ambapo hadi sasa analima hekta tano.
Mkulima huyo amesema awali alikuwa analima kilimo cha mazoea bila kutumia mbolea na kupanda mbegu za kienyeji na baada ya kushauriwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kuanza kutumia mbegu bora ya mpunga aina ya TXD 306 QDS amepata mafanikio makubwa.
Ameongeza kuwa katika hekta hizo tano alikuwa akipata mazao gunia 15 kwa hekta moja sawa na mgunia 75 ambapo kwa sasa anapata gunia 200.
"Kwenye maonesho haya SAGCOT imetugharamia kutuletea ili tuje tujifunze kwa kukutana na wakulima wenzetu," ameeleza.
Akizungumzia mafanikio yake yatokanayo na kilimo ameeleza kuwa amejenga nyumba ya vyumba sita na kupangisha Mafinga mjini ,kusomesha watoto wake pamoja na kununua Pawatila lenye thamani ya Sh milioni 12.
"Mimi ni mama mjane sijawahi kushindwa na maisha napambambana na kilimo na kufuata ushauri ninaopatiwa na SAGCOT pamoja na Wataalamu wengine wa kilimo," amesema.
Ameongeza kuwa SAGCOT imewapatia elimu ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao yao ambapo awali walikuwa wanauza bila kukoboa lakini kwa sasa wanauuza mchele hawauzi mpunga.
Aidha ametoa wito kwa wanawake ambao wanaogopa kujiingiza katika biashara ya kilimo huku akiwataka waondoe woga SAGCOT ipo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.
Naye mkulima wa viazi mviringo na parachichi kutoka Njombe Neema Mgaya amesema kuwa anatumia mbegu aina ya SAGITTA ambayo inamzalishia gunia 150 katika hekta moja.
Amesema awali kabla ya kutumia ya SAGITTA alikuwa akipata gunia 30 hadi 40 kwa hekta hiyo moja alipokuwa anatumia mbegu ambazo hajashauriwa na Wataalamu pamoja na SAGCOT.
"SAGCOT imetusaidia sana katika kilimo kwa ushauri na kwa sasa imetujengea banda la mbegu," amesema.
0 Comments