JWTZ LATOA SIKU SABA KWA RAIA WANAOVAA SARE ZA JESHI

Na Asha Mwakyonde,Dodoma 

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),limetoa siku saba kuanzia leo  kwa wanaovaa mavazi ya kijeshi au yanayoelekea kufanana na sare za Jeshi hilo kusalimisha mavazi hayo huku likisema baada ya siku hizo kuisha hatua kali zitachukuliwa.

Pia Wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi hayo na kuyauza kwa baadhi ya raia kupitia maduka yao au maaeneo ya biashara wametakiwa kuacha na baadhi ya wasanii wanaovaa  mavazi hayo bila kufuatwa utaratibu.

Akizungumza leo Agosti 24, 2024  jijini Dodoma  wakati akitoa ufafanuzi kuhusu sare hizo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda na Mnadhimu  Mkuu wa JWTZ Luteni Jenerali Salum Haji Othman, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi hilo, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema  kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya wanaokamatwa au kuonekana wakiwa wamevaa sare za Jeshi hilo.

Ameeleza kuwa kifungu cha 178 cha Sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 (Penal Code), na kifungu cha 6 cha Sheria ya Usalama wa Taifa, vinakataza raia kuvaa sare na mavazi ya Majeshi ya Ulinzi yanayofanana nayo. 


Luteni Ilonda ameyataja mavazi hayo kuwa ni kombati vazi la mabaka mabaka, Makoti, Tisheti, Suruali, magauni, kofia,viatu mabegi na kaptula zenye rangi zinazofanana au kushonwa katika mitindo ya kijeshi.

Ameongeza kuwa katazo hilo ni kwa nujibu wa kifungu cha 99 cha Sheria ya  Ulinzi  wa Taifa (NDA),sura ya 192  Sheria Namba 24 ya  mwaka 1966 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
 
"Wapo ambao wanayatumia mavazi haya  kufanya utapeli kwa wananchi na wengine kufanya vitendo viovu  wamekuwa wakidhaniwa kuwa ni wanajeshi. Hivyo vitendo hivi ni vya uvunjifu  wa sheria za nchi havipaswi kufumbiwa macho.Hali  hii ikiachwa inaweza kuhatarisha Ulinzi na usalama wa nchi yetu," ameeleza.

Aidha Jeshi hilo limewaomba wananchi kuendelea kuliunga mkono  ambalo daima liko imara na tayari kulitimikia  kwa uaminifu mkubwa serikali.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Gerson Msigwa amewataka wazazi kuhakikisha wanakagua mabegi ya watoto ili kusalimiasha Sare hizo pindk wanapozikuta ndani ya siku zilizotolewa.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU