TARURA: KM 21,057.06 KUFANYIWA MATENGENEZO


Na Asha Mwakyonde,Dodoma

JUMLA ya barabara zenye urefu wa kilometa 21,057.06 zitafanyiwa matengenezo, kilometa 427 zitajengwa kwa kiwango cha lami, kilometa 8,775.62 zitajengwa kwa kiwango cha changarawe, madaraja na makalavati 855 yatajengwa pamoja na mifereji ya mvua kilometa 70 katika mwaka wa fedha 2023/24.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumuna mwelekeo wa Wakala huo katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 amesema jumla ya shilingi bilioni 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya. 

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 710.31 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.

"Mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi. Hadi Machi, 2023 TARURA imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya shilingi bilioni 8.7 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50,"amesema Mtendaji huyo. 

Amefafanua kuwa madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Morogoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15.

Mtendaji huyo ameeleza kubwa wanaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine ya mbali na kwamba Teknolojia hizo ni pamoja na ECOROADS, Ecozyme, na GeoPolymer. 

"Hadi sasa kwa kutumia teknolojia ya ECOROADS, katika Jiji la Dodoma imejengwa kilometa 1 ambayo imekamilika na katika Wilaya ya Mufindi zitajengwa kilometa 10 na Mkandarasi yuko kwenye matayarisho ya kuanza kazi," amesema.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO Gerson Msigwa ameeleza kuwa dhamira  ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni  kuhakikisha taasisi zote za Serikali zinazofanya biashara na zisizofanya biashara zinafanya kazi zake kwa tija.

TARURA imeanzishwa mwaka 2017 lengo likiwa ni kupanua mawanda ya namna ambavyo tutawahudumia Watanzania kwa kuwaboreshea barabara.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI