Na Asha Mwakyonde,MbeyaBODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imeweka lengo la kuzalisha tani 120,000 za singa za Mkonge ifikapo mwaka 2025 ili kukidhi mahitaji ya soko la dunia kutokana na maboresho ya zao hilo yaliyofanywa na Bodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa bodi hiyo, Esther Mbussi, amesema uzalishaji wa mkonge kwa sasa tani ni 48,000.
Amesema kuwa Bodi hiyo imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji ambayo ni kugawa miche bure kwa wakulima katika wilaya mbalimbali nchini, kununua mitambo ya kuchakata mkonge wa wakulima, utafutaji masoko, kutoa elimu na kuhamasisha wakulima wengi kulima zao hilo.
“zao la mkonge ni la kimkakati na matumizi yake ni makubwa ndani na nje ya nchi lengo letu kama Bodi ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka kutokana na mikakati tuliyojiwekea kama Bodi," ameeleza Mbussi.
Naye Ofisa Kilimo katika bodi hiyo, Emmanuel Lutego, ameeleza kuwa kilimo cha mkonge ni fursa kwa wakulima kutokana na kuhimili hali ya ukame inayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameongeza kuwa zao hilo tangu kupandwa hadi kufikia uvunaji unachukua kipindi cha miaka mitatu na uvunaji wake ni miaka 18 na kwamba huvunwa kwa mwaka mara mbili.
0 Comments