VETA DAR YABUNI MTAMBO WA KUCHAKATA MAZIWA KUWA UNGA

Na Asha Mwakyonde, Mbeya 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA),kupitia Chuo cha Ufundi Stadi Veta Dar es salaam imebuni na kutengeneza Mtambo wa kuchakata maziwa na kuyaongezea thamani kwa kuwa unga

Akizungumza Agosti 6, 2023 katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya, amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutengeneza maziwa ya unga kutoka maziwa ya maji Mkufunzi Emmanuel Bukuku amesema waliona maziwa hayo yakiongezewa thamani na kuwa katika mfumo wa unga yanaweza kusafiri kirahisi.

“Niligundua wafugaji wengi wanapeleka maziwa kwenye vyama vya ushirika lakini wakati mwingine vyama vinashindwa kuyanunua yote na mengine huharibika.

Mwalimu huyo amesema mashine hiyo ina uwezo wa kutengeneza lita nane za maziwa ya maji na kupata kilo moja ya maziwa ya unga kwa dakika nane mpaka 10.

Amesema mashine hiyo inafanya kazi vizuri kwani tayari wameifanyia majaribio ambapo wanatarajia kuipeleka kwenye maeneo ambayo maziwa yanapatikana kwa wingi.

“Tuenaona mashine hii inaweza kufanya kazi vizuri mfugaji akapata faida ni mikoa ya Mbeya eneo la Tukuyu ambapo lita moja ya maziwa inauzwa kati ya Sh 500 mpaka Sh 1,000 na maeneo ya Njombe na Shinyanga,” amesema.

Amesema mashine hiyo yenye thamani ya Sh milioni 6 ina uwezo wa kuchakata mapipa mawili ya maziwa kwa siku moja.

Amesema kwa viwanda vikubwa wakipata wateja wanaweza kutengeneza mashine kubwa zaidi ya hiyo.

“Wafugaji wakitumia mashine hii watapata faida kubwa na inaweza kuwekwa kwenye vituo vya kukusanya maziwa. Maziwa ya maji yanauzwa wastani wa Sh 1,100 kwa lita lakini kilo moja ya maziwa ya unga inauzwa Sh 18,000,” amesema Bukuku.

Hivyo kilio cha wafugaji kukosa masoko ya uhakika ya maziwa huenda kikawa historia baada ya Chuo cha Ufundi Stadi Veta kutengeneza mtambo wa kuyaongezea thamani. 

Post a Comment

0 Comments

DKT. BITEKO ASISITIZA UMUHIMU WA MIFUMO THABITI YA NISHATI JADIDIFU KUKIDHI MAHITAJI YA NISHATI