VETA MASHINE YA KUCHAKATA CHAKULA CHA KUKU

Na Asha mwakyonde,Mbeya

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kupitia Chuo cha Ufundi Stadi Veta Songea kimetengeneza mashine ya kuchakata chakula cha kuku na samaki kilicho kwenye mfumo wa punjepunje.

Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya Mkufunzi wa Chuo cha Veta Songea, Sussack Mbulu, ina uwezo wa kuzalisha kilo 100 kwa siku.

Amesema mashine hiyo ni rahisi kutumiwa na wafugaji wadogo wadogo kuzalisha chakula badala ya kutegemea mashine kubwa.

“Chakula kinakuwa kwenye mfumo wa punjepunje kwa sababu virutubisho vyote vinajumuishwa kwenye kipande kimoja, kuku au samaki akila kitamfanya awe na afya njema kuliko utaratibu uliokuwa ukitumika siku za nyuma wa kupalaza mahindi na kuweka kwenye mfumo wa chengachenga.
 
“Teknolojia hii itapunguza gharama za ununuzi wa chakula na hata kwa wanafunzi wetu wanaweza kujiajiri kwa kutengeneza mashine au kuuza chakula,” amesema. 

Ametoa wito kwa jamii kutembelea vyuo vya Veta ili kujifunza na kupata mashine hizo kisha kujiajiri na kuongeza kipato kwa vijana na wanawake ambao wengi ni wafugaji. 

“Kwa wanaofuga samaki hii ni fursa kwa sababu mashine hii inatengeneza chakula ambacho kinaelea,” amesema. 

Kwa mujibu wa Mbulu, mashine hiyo inauzwa kwa Sh 300,000 na tayari watu mbalimbali wameomba kutengenezewa. 

Mmoja wa wakulima na mfugaji kutoka Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Zuberi Paulo, amesema amekuwa akipata changamoto ya magonjwa ya kuku na vyakula hasa upatikanaji wa soya. 

“Kuna changamoto ya upatikanaji wa vyakula vya kuku na namna ya kuvichanganya, nikiwa na mashine hii itanisaidia kurahisisha zoezi la uchanganyaji na kupata chakula ambacho ni kikavu,” amesema Paul.

Post a Comment

0 Comments

ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA