Na Asha Mwakyonde,Mbeya
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA), imetakiwa kuhamasisha wakulima waanze kuungana kupitia vyama vya msingi vya ushirika na hata vikundi ili iwe rahisi kuweza kuwa na kauli moja pindi wanapouza mazao yao ili kupata bei nzuri ya kuuza mazao hayo.
Hayo yamesemwa jijini Mbeya leo 5, 2023, na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alipotembelea banda la Wakala huo katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani hapa katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula'.
Kigahe amesema serikali inaamini wakiwa kwenye vikundi, ushirika na vyama vya msingi ni rahisi kutoa huduma ya kuwakopesha mzani ili kila anayekwenda kununua mazao yao apime ndio akafungashe vizuri kama kadri ya maelekezo yanavyotakiwa.
"Nakushukuru Mkurugenzi kwa kazi kubwa unayoendelea kuifanya lakini tutaongea na wenzetu Wizara ya Kilimo tuendelee kushirikiana kuhamasisha wakulima kuwa kwenye vikundi kwani mtu mmoja mmoja sio rahisi mtu kuwa na mzani na kumlazimisha mnunuzi kununua kwa vipimo," amesema.
Ameongeza kuwa serikali imepiga hatua kwenye baadhi ya mazao na maeneo mengine.
Awali Mkurugenzi Huduma za Biashara kutoka WMA, Deogratias Maneno amesema kimsingi ili waondokane na suala la rumbesa lazima upimaji kwa kutumia mzani uwepo ndio suluhisho la kudumu.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa suala la mizani lilikuwa tatizo wananchi walikuwa wanashindwa kununua lakini kwa sasa zipo za kutosha wanaweza kujiunga kwenda vikundi na wakanunua kwa pamoja ni suala la kuweka utaratibu wakapewa elimu.
Kwa mujibu wa Maneno kwenye mazao ya kimkakati wamejiwekea utaratibu wanashiriki kila zoezi katika mazao kama pamba na korosho kutoa elimu.
Ameongeza kuwa kwenye zao la pamba kulikuwa na mgogoro mkubwa na kwamba katika eneo ambalo serikali wanajivunia ni upande wa zao hilo.
Amesema katika zao hilo kwa sasa wanazungumzia bei sio suala la vipimo wanashirikiana kama serikali kwa pamoja.
0 Comments