Na Asha mwakyonde, Mbeya
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imewashauri wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutembelea banda la mamlaka hiyo ili kupata elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya waone picha, dawa halisi lengo likiwa ni kuweza kukabiliana na mapambano dhidi ya dawa hizo.
Akizungumza jijini hapa leo 2, 2023, katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nane nane), ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale yenye kaulimbiu isemayo 'Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula', Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka DCEA, Florence Khambi amesema kuwa uwepo wao katika maonesho hayo wananchi wanapata fursa ya kuziona dawa halisi za kulevya.
Khambi ameeleza kuwa bangi ni uoto wa asili unaweza kuota sehemu yoyote ile, hivyo mwananchi akiuona aweze kuung'oa na asipo ung'oa mbegu yake ikikua na kukomaa itaweza kusambaa na kuenea katika maeneo mengine.
"Kwanini tunaonesha mmea wa bangi hapa ni kwa sababu ni uoto wa asili unaweza kuota sehemu yoyote ile, hivyo mwananchi yoyote akiuona aung'oe na asipo ung'oa mbegu yake ikikua na kukomaa itaweza kusambaa na kuenea katika maeneo mengine, tumeonesha ili mwananchi aweze kuujua hasa waliopo vijijini kwenye milima inaweza kusafirishwa na maji kwenda kwenye maeneo yao," ameeleza.
Ameongeza kuwa kuna dawa nyingine za viwandani zinasafirishwa kuingizwa nchini zikiwamo Kokeini, Heroin wananchi watapata kufahamu namna zinavyofungwa na kusafirishwa endapo watatembelea katika banda hilo.
Afisa huyo amesema wanawapatia wananchi waliotembelea katika banda la mamlaka hiyo ufahamu kuhusiana na dawa hizo hasa zinazoingizwa ili waweze kumtambua mfanyabiashara wa dawa na wao waweze washiriki katika mapambo ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya.
0 Comments