MATUMIZI YA TEHAMA KUCHAGIZA UFANISI KATIKA KUKABILIANA NA MAAFA


Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya African Dream tarehe 04 Oktoba, 2023 Jijini Dodoma.

Baadhi ya wajumbe wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa wakifuatilia kikao hicho

Afisa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Bw. Felix Makundi akiwasilisha mada kuhusu Sheria na Miongozo ya Serikali wakati wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa.

Afisa TEHAMA Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Alex Ndimbo akiongoza kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa.

Afisa TEHAMA na Mratibu wa Maafa kutoka Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Yona Benjamin akichangia jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijiti wa usimamizi wa maafa, mara baada ya ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika Ukumbi wa hoteli ya African Dream Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Na Mwandishi wetu- Dodoma

SEKTA na Taasisi zinazohusika na masuala ya dharura zimehimizwa kutumia Jukwaa la Kidijitali lenye lengo la kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kubaini kuwepo kwa viashiria vya majanga na kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa pamoja na maafa yanayoweza kudhuru maisha, mali na mazingira.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Luteni Kanali Selestine Masalamado wakati akifungua Kikao Kazi cha kujadili mapendekezo ya mfumo shirikishi wa kidijitali wa usimamizi wa maafa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya African Dream Oktoba 4, 2023 Jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema uwepo wa mfumo huo utawezesha mawasiliano na kutoa taarifa kwa waratibu wa maafa katika eneo husika ili kuchukua hatua kwa haraka kuokoa maisha na mali akisema Idara imekuwa ikiboresha utaratibu wa kupokea na kutoa taarifa za maafa kutoka kwa umma na wadau kwa ajili ya usimamizi wa maafa pamoja na maboresho ya mifumo ambayo inatumika kuratibu taarifa husika.   

“Ni wazi kuwa kumekuwa na majanga au maafa katika maeneo mengi kama mafuriko, moto, ukame, matetemeko ya ardhi, milipuko ya magonjwa (wanyama, binadamu na mimea) hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Taasisi ya The Southern African Centre for Infectious Disease Surveillance (SACIDS) Foundation for One Health tuliandaa  jukwaa la Kidijitali lenye lengo la kuimarisha uwezo wa kitaifa wa kubaini kuwepo kwa viashiria vya majanga,” Amesema Luteni Kanali Masalamado.

Aidha ameeleza kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa ina jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa 2004, kupitia Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya Mwaka 2022, Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa pamoja na Mipango na Miongozo mbalimbali.

“Sehemu ya Pili, Kifungu cha 4(2)(i) kimeelekeza kuwa Idara ya Menejimenti ya Maafa itaweka mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano utakaowaunganisha wadau wa masuala ya maafa, kufuatilia mwenendo wa majanga na hali ya maafa kwa ajili ya kuchukua hatua za kuzuia na kukabiliana na maafa kwa wakati,” Amefafanua.

Post a Comment

0 Comments

 MAGARI 25 YA TUME YA MADINI YAMEZINDULIWA,YATASAMBAZWA KWENYE OFISI ZA MAAFISA MADINI