Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SERIKALI imesema itaendelea kuwekeza na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya Nukta Nundu (Breli) pamoja na teknolojia saidizi ili kuhakikisha watu wasioona wanapata fursa sawa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini hapa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, wakati akitoa tamko kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Breli yanayofanyika leo kitaifa mkoani Tanga.
Nderiananga amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa watu wasioona katika jamii na itaendelea kuthamini nafasi yao kwa kuzingatia kaulimbiu ya kutomwacha mtu nyuma katika mchakato wa maendeleo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi, taasisi za umma na binafsi pamoja na mashirika ya kiraia kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira jumuishi yatakayosaidia kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha wasioona na kuhakikisha wanapata haki na fursa sawa kama wengine.
Ameeleza kuwa Siku ya Kimataifa ya Breli imeanzishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuyapa mataifa fursa ya kutafakari umuhimu wa teknolojia ya Breli katika kuwawezesha watu wasioona kushiriki kikamilifu katika elimu, mafunzo ya ujuzi na maendeleo kwa ujumla.
“Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hii. Kwa utaratibu wa kitaifa, maadhimisho hufanyika katika halmashauri zote nchini huku kitaifa yakifanyika mkoani Tanga. Mwaka huu kutakuwa na maonesho ya teknolojia na kazi za wasioona, upimaji wa elimu na ujuzi, kongamano la wadau pamoja na burudani na hotuba za viongozi,” amesema.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Teknolojia ya Breli Husaidia Kuchochea Maendeleo kwa Wasioona na Ujenzi wa Taifa.”
Amesema kaulimbiu hiyo inaonesha namna Breli inavyowawezesha wasioona kushiriki katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia, hivyo kuchangia maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Nderiananga amebainisha kuwa maadhimisho hayo pia yanatambua mchango wa Louis Braille, mwanzilishi wa mfumo wa maandishi ya Breli, ambao umebadilisha maisha ya mamilioni ya watu duniani kwa kuwawezesha kusoma, kuandika na kupata taarifa kwa usawa na wanaoona.
Akizungumzia jitihada za Serikali, amesema zimeendelea kuwekwa sera, sheria na mikakati mbalimbali ya kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu, hususan wasioona.
Ametaja miongoni mwa nyenzo hizo kuwa ni Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023), Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura ya 183, zinazolenga kuimarisha usawa na ujumuishwaji.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Mkoa wa Dodoma, Enock Mbawa, aliiomba Serikali kuendelea kuwashirikisha katika programu mbalimbali na kuhakikisha wanapatiwa vifaa vitakavyowawezesha kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Amesema ushiriki wao katika sekta mbalimbali ni muhimu katika kufikisha sauti zao na kwamba maadhimisho hayo yatasaidia kuimarisha mshikamano miongoni mwao na wadau wengine.
Aidha, ameishauri jamii kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu akisisitiza kuwa vifaa vya kujifunzia vinapatikana na vinaweza kuwasaidia kufikia malengo na ndoto zao.





0 Comments