WADAU WA KILIMO AFRIKA WATAFUTA SULUHISHO LA KUONGEZA TIJA YA UZALISHAJI


Na Asha Mwakyonde

TANZANIA imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (ACSAM) uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026, ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka mataifa ya Afrika na sehemu nyingine duniani kujadili namna bora ya kuendeleza matumizi ya teknolojia na zana za kisasa katika shughuli za kilimo.

Mkutano huo uliandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO),kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, watafiti, sekta binafsi pamoja na taasisi za maendeleo ili kuharakisha matumizi ya zana na teknolojia za kilimo zinazoweza kuongeza tija na uzalishaji kwa wakulima barani Afrika.

Kupitia mkutano huo, washiriki walipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu sera na mikakati ya kukuza matumizi ya mashine na teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao, sambamba na kutafuta suluhisho la changamoto zinazokwamisha maendeleo ya kilimo katika nchi nyingi za Afrika.

Ajenda mbalimbali zilijadiliwa katika mkutano huo, ikiwemo namna ya kuboresha upatikanaji wa zana za kilimo, kuimarisha utafiti na ubunifu katika teknolojia za kilimo, pamoja na kuhamasisha matumizi ya mifumo ya kilimo cha kisasa na kidijitali. 

Aidha, wadau walijadili mikakati ya kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija na ushindani wa uzalishaji wa mazao.

Mbali na mijadala, mkutano huo pia ulihusisha maonesho ya mashine na vifaa vya kisasa vya kilimo, huku programu maalum kwa vijana zikilenga kuwahamasisha kushiriki katika biashara na huduma zinazohusiana na matumizi ya zana za kilimo.

Waandaaji wa mkutano huo walisema ACSAM ni jukwaa muhimu linalosaidia kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta ya kilimo barani Afrika, kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kisasa kinachoweza kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi za Afrika.

Post a Comment

0 Comments

MAPINDUZI YA KIDIGITALI CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA YAMVUTIA WAZIRI HOMERA