ANATROPIA AHOJI UPATIKANAJI BURE WA KITITA CHA WAJAWAZITO

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum  Anatropia Theonest ameihoji Serikali  namna ambavyo inaweza kuwasaidia kitita  cha kujifungulia wanawake wanaoshindwa kumudu kitita hicho wakati wa kujifungua.

 Anatropia ametoa kauli hiyo leo Feb 6,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiuliza swali la msingi ambapo ametaka kujua wanawake wangapi wamesaidiwa huduma hiyo.

"Je  ni Wanawake wangapi wameshindwa kumudu Delivery Kit na kupewa Vifaa hivyo na Hospitali au Kituo cha Afya husika.?"amehoji Anatropia

Akijibu swali hilo  bungeni Naibu Waziri Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Dk. Festo Dugange amesema kuwa  Serikali inaendelea kutoa huduma za afya kwa wajawazito wanaojifungua kwa kuzingatia Sera ya afya ya mwaka 2007.

Amesema Sera hiyo imeainisha makundi ya matibabu kwa msamaha ikiwemo huduma ya wajawazito na kujifungua. Katika kipindi cha miaka miwili (2022 na 2023) jumla ya wajawazito 2,707,098 walijifungua kwenye vituo vya kutolea huduma ngazi ya Msingi.

"Moja ya huduma inayotolewa katika vituo ni kitita cha kujifungulia (delivery kit) kwa wajawazito wasiomudu.," ameeleza Dk. Dugange.

 Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2022 na 2023 jumla ya wajawazito 10,829 walipewa vifaa vya kujifungulia katika vituo vya huduma za afya ya Msingi na kuwawezesha kupata huduma hiyo.

Aidha katika maswali ya nyongeza Anatropia amesema " tukubaliane suala la kujifungua haipaswi kuwa ni kifo na kupona Tanzania ni moja ya nchi tano chini ya jangwa la Sahara  linaloongoza kwa vifo vya wajawazito  na vifo vingi vinasababishwa na magonjwa ya kuambukiza ambayo yanapatikana wakati  wa kujifungua kwa kukosa maji na vitu vyenye usafi. Ni kwa nini Delivery Kit  zisitolewe bure kwa wajawazito ili kupunguza idadi ya magonjwa kwa wanawake wakati wakijifungua? 


Katika swali lingine alihoji kwa nini lisitengwe fungu la fedha maalum kwa ajili ya kuwapatia akina mama kununua Delivery Kit kwa lengo la kuweza kuokoa maisha ya akina mama hao amboa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua?

Naibu Waziri Dugange amesema katika nchi suala la kujifungua na kifo si mambo kwa sasa ambayo yapo karibu ikumbukwe mwaka 2016  kurudi nyuma vifo vya wajawazito vilikuwa 556 kati ya vizazi hai 100,000 .

Amefafanua kuwa baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuweka vipaumbele vya ujenzi wa vituo vya afya, Zahabati , vifaa na tiba pamoja na DAWA vifo hivyo vimepungua kutoka 556 hadi kufikia 104 katika vizazi hai 100,000 na kazi inaendelea.

" Kwa uwekezaji huu mkubwa kwa wizara ya afya na ofisi ya TAMISEMI katika vituo vya afya na watumishi wanaokwenda tuna uhakika Tanzania itakuwa ni miongoni mwa nchi zenye vifo vichache  vinavyotokana na kujifungua, nikuhakikishie Mheshiwama mbunge kitita hicho kinatolewa bure  kwa wajawazito wote kwa sababu wanazikuta kwenye Zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu  lakini suala la kujifungua linatokea wakati wowote ndio maana tunatoa maelekezo kuwa na vifaa hivi nyumbani," amesema.

Naibu Waziri Dugange amesema ili ikitokea lolote mama huyo asiweze kupoteza maisha  na mtoto.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU