Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum katika mwaka 2024/2025, kupitia Idara na Taasisi zilizo chini yake itatekeleza vipaumbele sita ili kuboresha utoaji wa huduma za maendeleo na ustawi wa jamii.
Akiwasilisha hotuba yake ya Mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 leo Mei 17,2024 bungeni Jijini hapa Waziri wa wizara hiyo Dk.Dorothy Gwajima amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukuza ari ya jamii kushiriki katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo iliyoibuliwa ngazi ya Msingi.
Dk. Gwajima amesema vingine ni kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili, uwezeshaji wanawake kiuchumi, upatikanaji wa haki, ulinzi na malezi chanya ya watoto,kuratibu na kuimarisha utoaji wa huduma za msingi za ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Waziri huyo vipaumbele hivyo hivyo ni pamoja kutambua, kuratibu na kuendeleza Makundi Maalum wakiwemo wafanyabiashara ndogondogo,kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika Taasisi na Vyuo vya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuimarisha ushiriki na mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa.
Ameeleza kuwa katika kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa,Wizara kwa mwaka 2024/2025 imekadiria kutumia kiasi cha Shilingi 67,905,259,000. Kati ya fedha hizo, Shilingi 47,487,079,000 ni fedha za matumizi ya kawaida ambapo Shilingi 21,650,426,000 ni Fedha za Mishahara na Shillingi 25,836,653,000 ni fedha za uendeshaji wa ofisi.
"Shilingi 20,418,180,000 ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo Shillingi 18,025,673,000 ni fedha za ndani na Shillingi 2,392.507,000 ni fedha za nje," ameeleza Dk. Gwajima.
Aidha Dk. Gwajima ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yaliyotengewa fedha kwa mwaka 2024/25 ni pamoja na eneo la kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi (Generation Equality Forum - GEF), kiasi cha shilingi bilioni 3.2 zimetengwa.
"Katika eneo la kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kiasi cha Shilingi bilioni 3.15 kimetengwa," amesema Waziri huyo.
Amesema maeneo mengine katika eneo la kutambua na kuratibu shughuli za kiuchumi za Makundi Maalum hususan wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo machinga, mama/baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji na ma makundi mengine yenye biashara ndogo halali zilizosajiliwa, kiasi cha Shilingi bilioni 10.5 kimetengwa kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili kuongeza mitaji na kuboresha shughuli zao za kiuchumi.
0 Comments