TAEC KUENDELEA KUPIMA MAJI YA VISIMA NCHI NZIMA

Na Asha Mwakyonde Dar es Salaam 

TUME ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC),imesema kuwa inaendelea na zoezi kupima maji ya visima nchi nzima ambapo linatekelezwa kupitia Sheria ya Nguvu za Atomu namba 7 ya mwaka 2003 lengo likiwa ni kubaini kama kuna viasili vya mionzi.

Wananchi wameombwa wananchi watoe ushirikiano kwa wakaguzi wanaopita katika maeneo mbalimbali kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa vizuri. 

Akizungumza Julai 5,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TAEC, Peter Ngamilo, ameeleza kuwa chini ya ardhi kuna madini ya Uranium ambapo maji yanaweza kuchimbwa na kukutana na madini ya mionzi ambapo mwananchi anaweza asijue.

Katika hatua nyingine amesema kuwa wanatoa vibali vya uingizaji, usafirishaji, umiliki wa vyanzo vya mionzi nchini, kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo yanayotumia vyanzo vya mionzi na kupima viasili vya mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa ili kulinda wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

Amesema Moja ya jukumu lao ni kufanya kazi ya kupima viwango vya mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanaokaa karibu waendelee kubaki salama dhidi ya madhara ambayo yanaweza kusababishwa na mionzi.

Ngamilo amebainisha kuwa wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwa kutumia vyanzo vya mionzi katika shughuli zao za kila siku, kwenye vituo vya afya, migodi, bandari, viwanja vya ndege kuna wafanyakazi wanatumia vyanzo vya mionzi katika shughuli zao za kila siku…moja ya kazi yetu ni kuhakikisha kwamba 

"Tunawaangalia wale wafanyakazi ili waendelee kubaki salama dhidi ya madhara ya mionzi," ameeleza Ngamilo.

Afisa Tafiti wa tume hiyo, Dk. Lazaro Meza, amesema mionzi inasababisha magonjwa ya saratani na mengine na kushauri wanaochimba visima kupeleka sampuli za maji katika tume hiyo ili zipimwe kujua kama maji yako salama au yana viasili vya mionzi.

“Ikitokea umechimba maji katika eneo lenye viasili vya mionzi kama mwananchi wa kawaida utajua kwa kuchuku sampuli ya maji na kuleta kwetu ili tupime tuangalie kama yako salama au yana viasili vya mionzi…kama maji yana uchafuzi wa mionzi kuna uwezekano mkubwa hata vyakula vikapata ndiyo maana kuna umuhimu wa kupima maji,” amesema Dk. Meza. 

Tume hiyo inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya mionzi na madhara yanayoweza kupatikana.

Post a Comment

0 Comments

 KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YANOLEWA