Na Asha Mwakyonde,Dodoma
TAASISI ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), ina mchakato wa kuingia makubaliano na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuendeleza kituo cha mafunzo ya wakulima cha Bihawana ili kiwe kituo bora kwa kilimo hai Ikolojia nchini.
Mwaka jana serikali ilizindua mkakati wa Kilimo Hai Ikolojia ambopo TOAM ni Sekretarieti ya kikosi kazi katika kutengeneza mkakati huo.
Pia TOAM ni Taasisi Mwamvuli ya mashirika mbalimbali yanayojohusisha na kilimo hai Tanzania ambapo ina wanachama zaidi ya 120 kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Haya ameyasema leo Agosti 8,2024 na Mtendaji Mkuu wa TOAM, Bakari Mongo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la taasisi hiyo kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nane nane ambayo yanaendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma amesema
wana vituo vingi na kwamba cha Bihawana wamepewa na Wizara ya Kilimo kuisimamia na kuiendeleza ili kiwe ni moja ya kituo bora kwa mbengu za asili (organically culture).
Mtendaji huyo ameeleza kuwa TOAM ikiwa ni Taasisi Mwamvuli imeweza kushiriki katika kutengeneza mkakati wa kilimo Hai Ikolojia kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.
Mongo amesema kuwa wameweza kuweka kipaumbele cha kuwa na maeneo sita kati ya 12 ya kuanza nayo katika mkakati wa Kilimo Hai Ikolojia.
Mtendaji huyo amefafanua kuwa eneo la kwanza ni upatikanaji wa pembejeo za kilimo hicho, utoaji wa maarifa ya kilimo hai Ikolojia huku akisema eneo jingine ni masoko ya kilimo hicho, eneo la Ardhi ni kwa namna gani ardhi hiyo itakuwa inatumika kwa uzalishaji wa kilimo hai Ikolojia.
Ameongeza kuwa eneo la sita ni uratibu ambapo linahitaji kuwa na uratibu thabiti ili waweze kuhakikisha wadau wote wanaotengeneza kilimo hicho wanatekeleza kwa ufanisi.
Aidha ameishukuru serikali ya Rais Dk Samia suluhu Hassan kwa kuwapatia nafasi hiyo na kwa ajili ya kusaidia zoezi zima la kutengeneza mkakati wa Kilimo Hai ambao utasaidia kusukuma maendeleo ya kilimo hicho Tanzania.
"Tunaishukuru Wizara ya Kilimo hususan Rais Dk Samia kwa kuweka nguvu kubwa kuendeleza sekta ya kilimo nchini ikiwamo kilimo hai Ikolojia, " ameongeza na kusema.
" Tupo hapa kwenye maonesho haya kuonesha bidhaa mbalimbali kwa kushirikiana na wakulima," ameeleza Mtendaji huyo.
Akizungumzia idadi ya wanachama hao amesema kuwa wamewagawa katika Kanda kuu tano ambazo ni Kanda za Nyanda za juu Kusini, Kanda ya ziwa ,kanda ya Kasikazini, Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kati.
Mtendaji huyo ameeleza kuwa lengo la kugawa Kanda hizo ni kurahisisha mawasiliano kwa wanachama wao.
Kwa upande wake mkulima wa Kilimo Hai kutoka kijiji cha Nzali Kata ya Chilonwa Wilaya ya Chamwino Dodoma Anastazia Madege amesema kuwa ameanza kilimo hicho tangu 2014 ambapo amepata faida kwa kuwa na chakula cha kutosha.
Amefafanua kuwa chakula anachokipata kupitia kilimo hicho kina ladha ya asili huku akieleza tangu alipoanza kilimo hai hajawahi kupoteza mbegu za asili.
0 Comments