Na Asha Mwakyonde DODOMA
SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),limesema kuwa limepokea changamoto katika Makundi mbalimbali ikiwemo viwango mbalimbali vya tozo katika mnyororo wa usafirishaji mizigo yao kwa njia ya bahari, ucheleweshaji wa meli kupata eneo la gati, uchelewaji wa magari katika mipaka yetu ambayo yanachukua mizigo bandarini na kwenda nchi jirani.
Pia TASAC, limesema kuwa limejidhatiti kuhakikisha huduma za usafirishaji kwa njia ya maji zinatolewa kwa ubora, ufanisi na kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo Agosti 8,2024 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nelson Mlali alipozungumza na waandishi habari kwenye banda lao lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kuwa kutokana na changamoto hizo wanakutana na wadau wao kwa lengo la kujaribu kuangalia namna bora ya kuweza kupunguza tozo ili kuzifanya bandari zisiwe ghali kutumika kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza ili waweze kumudu ushindani katika bandari zao na kuhakikisha huduma za usafirishaji zinatolewa kwa ubora na ufanisi.
"Tunaomba ushirikiano wa wananchi hasa wale walio karibu na maji, Pwani za bahari, fukwe au maziwani wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanakuwa salama ili kudumisha usafiri kwa njia ya maji," amesema.
Ameongeza kuwa mojawapo ya kazi za TASAC ni kusimamia sekta ya usafiri kwa njia ya maji, ambapo wana jukumu la shughulika na meli pamoja na mizigo.
Shirika hilo limetoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na fukwe au maziwa wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama ili kudumisha usafiri kwa njia ya maji.
0 Comments