NIC YAWASHAURI WAKULIMA KUTUMIA BIMA YA KILIMO KUJIKINGA NA MAJANGA


Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

WAKULIMA wameshauriwa kuacha kulima kilimo cha mazoea,kiholela ambacho hakijalindwa na bima ya kilimo (Mazao na Mifugo),hadi kilindwe lengo likiwa ni kulinda uchumi wa mkulima mmoja mmoja uwe imara ili kukuza uchumi huo kwa wakulima hao na taifa kwa ujumla.

Akizungumza leo Agosti 3,2024, waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima na wafugaji nane nane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Shirika la Bima la Taifa (NIC),Karimu Meshack amesema kuwa kazi ya Rais Dk. Samia suluhu Hassan inakuwa rahisi kwa kuwa uchumi wa nchi upo katika mikono salama.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa uchumi huo hauwezi kupotea ambapo ikitokea majanga yoyote kwenye kilimo NIC inamrudishia mkulima kile alichokuwa amekiwekeza katika kilimo.

Amesema wananza kulinda kilimo kwenye shamba lenye ukubwa kuanzia hekta 100 huku akifafanua kuwa wanatambua wakulima wengi wanalima maeneo madogo madogo NIC inawaweka katika makundi, vyama vya msingi ili kupata hekta hizo ambazo zitapatiwa bima hiyo.

" Kama mkulima amewekeza milioni 500 sisi tunamrudishia ili alime tena na akiwa hajakata bima ile milioni 500 inakuwa imepotea na itamgharimu kwenda kumitafuta ili aende akalime, tupo kwenye haya maonesho kwa ajili ya kutoa elimu na kuwashawishi wakulima waweze kulima salama kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi," alisema.

Ameongeza kuwa kupitia bima hiyo tayari Mkoa wa Kilimanjaro baadhi ya wakulima wameshanufaika na bima hiyo ambapo NIC iliwalipa zaidi ya milioni 255 ili warudi shambani wakalime.

Aidha Meshack amesema kuwa mwitikio wa wakulima kwenye bima hiyo ni mkubwa kulingana na muda wa bima kuanza kutolea kwa wakulima hao.

"Kila mwaka tumekuwa tukishiriki maonesho ya wakulima nane nane na mwaka huu tupo katika maonesho haya ambayo yanaonekana kuwa ni mazuri, yupo hapa kutoa elimu " alisema Meshack.

Akizungumzia maonesho hayo amesema kuwa wamekuja na bidhaa mbalimbali kama NIC ambao wanatoa huduma za bima za maisha, mali na ajali.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kwa upande wa bima za mali na ajali wana bima za kilimo na mifugo kwa kuwa maonesho hayo ni mahususi kwa ajili ya wakulima na wafugaji.

Amefafanua kuwa wakulima wanatumia fedha nyingi kuwekeza kwenye kilimo na kwamba kilimo na mifugo vimeambatana na changamoto, viashiria na majanga ambavyo vinaweza vikaikumba kilimo na mifugo kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo amesema kwenye kilimo kuna mambo ya tabia nchi ambapo mkulima anaweza akalima na akakutana na ukame, mvua nyingi zilizokithiri zikaharibu mazao na wadudu.

Amesema NIC inataka mkulima alime na kwamba yale majanga

yanayoambatana na kilimo awaachie Shirika hilo ambapo mtaji aliyowekeza kwenye kilimo usipotee huku akisema kuwa wao wanamkinga mkulima huyo na majanga yatakayotokea.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI