VETA YAWAKARIBISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LAO NANE NANE DODOMA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetoa wito kwa wananchi kutembelea banda lao lililopo katika Viwanja vya maonesho ya Kilimo na Ufugaji (Nanenane) ili kuona fursa mbalimbali zinazopatikana katika mamlaka hiyo.

Akizungumza jijini hapa Afisa Mkuza Mitaala wa VETA, Anna Nyoni kwenye maonesho hayo yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma amesema kuwa wamekuja kuwaeleza wananchi fursa mbalimbali zinazopatokana VETA.

Ameeleza kuwa wanatoa mafunzo katika fani mbalimbali takribani 89 ambazo zimejikita katika sekta tofauti tofauti 13 ambapo Wana Sekta za Utalii, sanaa za maonyesho na mikono, ufundi vyuma, ufundi umeme, ususi na urembo, kilimo na usindikaji wa vyakula, uchapaji, huduma za biashara, ufundi magari pamoja na sekta ya uziduaji madini.

Amefafanua kuwa wanatoa mafunzo katika kozi za muda mrefu na kozi za muda mfupi ambapo kozi za muda mfupi zinaanzia mwezi mmoja mpaka miezi sita, na kozi za muda mrefu ni kwa miaka mitatu.

Amesema mwanafunzi anasoma miaka mitatu ambapo kuna ngazi ya kwanza hadi ya tatu na akifika ngazi ya pili anafanya mtihani wa kitaifa na kupatiwa cheti cha ngazi ya pili na akifika ngazi ya tatu pia anafanya mtihani wa kitaifa ambapo atapata cheti cha ngazi ya tatu.

"Kwahiyo pamoja na kwamba tuna hizo sekta nyingi na fani nilizozitaja, pia tuna sekta ya kilimo na usindikaji wa chakula na ndo hasa ambayo tunaitangaza hapa Nanenane. Katika sekta hiyo tuna fani mbalimbali ambazo ni kilimo cha mbogamboga na matunda, fani ya uchakataji wa miti, kilimo cha mazao ya nafaka, Bioenergy na fani ya utunzaji wa mifugo," amesema na kuongeza kuwa:

"Kwenye utunzaji wa mifugo tunasema kila kinachotoka sisi tunakitumia kwa mfano kinyesi cha Ng'ombe tunakibadilisha kinaweza kutumika kwenye kupikia na shughuli zingine mbalimbali. Hivyo hakuna tunachokitupa...pia tuna fani ya kuchakata nyama, fani ya kufuga nyuki pamoja na fani nyingi ambazo zinahusiana na masuala ya kilimo,".

Aidha ametoa wito kwa Watanzania kuwapeleka watoto wao kusoma Veta ili wapate Ufundi wa aina mbalimbali ambao utawasaidia huku akibainisha kuwa VETA ina vyuo vinavyofanya kazi 80 na wanampango mwakani wa kuongeza vyuo vingine 65.

Post a Comment

0 Comments

CHATANDA:RAIS DK. SAMIA AMEIMARISHA SEKTA YA MADINI