UDOM YAISISITIZA JAMII KUTUMIA WATALAAM WA LISHE WANAOTAMBULIKA

Na Asha Mwakyonde,Dodoma

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimesisitiza umuhimu wa kuwatumia wataalam wa lishe wanaotambulika ili kuepuka upotoshaji ambao unaweza kusababisha athari mbalimbali za kiafya kwenye jamii.

Hali hiyo inatokana na wimbi kubwa la watu kuibuka na kujiita wataalamu wa lishe kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mbalimbali kwa lengo la kujinufaisha bila kujali athari za watumiaji ambazo zinaweza kujitokeza.

Akizungumza Agosti 3,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma Mkufunzi Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma katika Idara ya Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii, Kassim Mohamed Ally, ameeleza kuwa Wataalam wa lishe wanaoibuka ni wengi hivyo jamii inapaswa kuwa makini na wanayoshauriwa.

Mkufunzi huyo amesema kuwa baadae watumiaji wanajikuta wanapata athari zikiwamo za vidonda vya tumbo na kwa upande wanawake wanaharibu mfumo mzima wa homoni.

Amesema wanatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora pamoja na kufanya uchunguzi wa awali wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Mkufunzi huyo amesema katika banda la UDOM wanafanya uchunguzi wa vipimo vya awali kama vile uwiano wa urefu na uzito, sukari, presha na vingine na kutoa ushauri juu ya suala zima la lishe.

“Tunatoa elimu ya tiba lishe kwa kutumia chakula ambayo inatoa mwongozo sahihi wa jinsi ya kula, wanafunzi wanasoma kozi hii kwa miaka minne kisha wanakwenda kwenye mazoezi ya vitendo hospitali au sehemu watakayochagua kwa mwaka mmoja,” amesema Ally.

Mkufunzi huyo amesema katika chuo hicho wanafunzi wanaosoma kozi hiyo wanafundishwa jinsi lishe inavyofanya kazi kwa kuunganisha na sayansi, muundo wa mwili na ufanyaji kazi wa mwili, uchakataji wa chakula mwilini.

Kuhusu uchunguzi wa awali wa afya amesema kesi nyingi wanazozipata ni watu kuwa na uzito mkubwa ambapo wamekuwa wakiwashauri jinsi ya kuupunguza kwa kuzingatia makundi muhimu ya vyakula.

Post a Comment

0 Comments

MAJALIWA: MJI KONDOA TUMEKUSANYA ZAIDI YA MILIONI 126 KIPINDI CHA JULAI HADI JUNI MWAKA HUU