WANACHI WAASWA KUACHA KUDANGANYIKA NA USHIRIKINA

Na WMJJWM, Tabora

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewaasa wananchi kuacha kudanganyika na imani za kishirikina kwa imani za kupata mafanikio.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Oktoba 23, 2024 wakati akizungumza na wananchi, kwenye Wilaya za Igunga na Nzega mkoani Tabora katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema matokeo ya imani hizo yanasababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwa watoto kuongezeka nchini, hasa ubakaji, ulawiti na mauaji hali inayoleta taharuki kwenye jamii kutokana na athari za maumivu na vifo.

"Waganga wa kienyeji wasiotambulika wanawadanganya kufanya mambo ya ajabu na ndio sababu wanafanya tiba zao kwa kificho. Pambaneni kufanya kazi badala ya kudanganywa na waganga hao" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Ameongeza kuwa, Serikali inapambana na ukatili ambao matokeo yake ni pamoja na kukosa huduma za msingi kama shule, zahanati, barabara, fursa za mikopo na maji, sekta ambazo zinatafsiri maendeleo na ustawi wa jamii na ndio zinazinduliwa katika ziara hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Chacha amebainisha baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni ikiwemo la binti kufariki wilayani humo baada ya kutolewa mimba ambapo wahusika wote wamekamatwa.

Mhe. Chacha amesema mkoa kupitia vyombo vya usalama, unashughulika kikamilifu na watuhumiwa wa ukatili na watahakikisha wanafikishwa kwenye mikono ya sheria wote watakaobainika.

Katika ziara hiyo katika Wilaya za  Igunga na Nzega, Waziri Dkt. Gwajima amekagua na kuzindua madarasa Shule ya Sekondari Mwayunge na Zahanati ya kijiji cha Nguriti wilayani Igunga na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa kalavati kwenye Kata ya Ijanija, Wilaya ya Nzega na miradi yote imegharimu  jumla ya shillingi milioni 500.5.

Post a Comment

0 Comments

WANANCHI ZAIDI YA 15,000 WA KATA YA MAKURO KUPATA MAWASILIANO YA SIMU