📍Asema msimu huu wa sikukuu ni fursa muhimu kwa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini
Na Mwandishi wetu,Dodoma
SERIKALI imewahimiza wananchi kutumia msimu wa sikukuu na likizo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kujifunza, kuburudika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Disemba 29,2024, na Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ernest Mwamwaja alisema Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vya kipekee ambavyo vinapaswa kuthaminiwa na Watanzania wenyewe.
“Msimu huu wa sikukuu ni fursa muhimu kwa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini ili kujivunia urithi wetu wa asili na kiutamaduni,”ameeleza.
Ameongeza kuwa:”Tulizindua kampeni maalumu ya kuhamasisha utalii wa ndani kati msimu huu wa sikukuu ijulikanayo kama “Funga mwaka kijanja talii “ ambayo inalenga kuwahamasisha watanzania wa rika zote kushiriki katika shughuli za utalii ambayo itakoma ifikapo junuari 10 mwaka huu.
Katika hatua nyingine Mwamwaja alisema TTB imejipanga kuendelea kushirikiana na waandishi wa habari ili kuongeza idadi ya watalii lengo ni kuhakikisha wanatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025 ya kufikia watalii milioni tano.
Amesema lengo lingine ni kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha sekta ya utalii inakua na kuchangia katika Uchumi wa taifa.
“Tunaamini kupitia waandishi wa habari tunaweza kuwafikia wananchi wengi na kutangaza vivutio vya utalii ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia za kutangaza vivutio vya utalii na kuongeza idadi ya watu wanaotembelea,”amesema
Ameongeza kuwa wanatamani kuona wananchi wanachangamkia fursa ya kutembelea vivutio vya utalii.
0 Comments