Dk.TULIA MGENI RASMI BONANZA LA MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA, WATUMISHI WA BUNGE


Na Asha Mwakyonde,DODOMA 

MWENYEKITI wa Bunge Bonanza, Festo Sanga,amesema bonanza la watumishi wa Bunge, na mashabiki wa michezo wa timu za Simba na yanga linalenga kukuza ushirikiano pamoja na kujenga afya za jamii ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.

Bonanza hilo linatajariwa kufanyika katika viwanja vya shule ya John Merlini ambapo litahudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),Wallace Karia, akiwa mgeni maalum.

Akizungumza jijini Dodoma leo Januari 30,2025 Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Bonanza hilo limeendelea kukua na kwamba mwaka huu linatarajiwa kuwa kubwa zaidi kuliko mabonanza yote yaliyopita.

"Tunataka kuona watu wakichangamkia fursa ya kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao, Pia, tunalenga kuimarisha mahusiano kati ya wabunge na watumishi wa Bunge kupitia michezo, Bonanza hili," amesema Sanga.

Amesema katika kuhakikisha bonanza linakuwa la mafanikio, waandaaji wake wamepanua wigo wa ushirikiano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, zikiwemo taasisi za serikali na binafsi kama DUWASA na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Meneja wa Azania Bank Tawi la Dodoma, Laiberia Peter, amesema benki hiyo imefadhili bonanza hilo kwa kutoa vifaa vya michezo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha mazoezi na kuchochea afya. 

"Tunahamasisha watu kufanya mazoezi kwa ajili ya afya zao, na pia tutatoa huduma zote za kibenki, ikiwemo kufungua akaunti na maelezo mengine, ameeleza.

Kwa upande wa timu ya Yanga, Afisa wa Chama na Matawi, Jimy Kidoki, amesema timu yao inaongoza kwa ushindi dhidi ya mpinzani wao na ameiomba Azania Bank kuendelea kuongeza michezo ili kuimarisha ushindani.

Ameongeza kuwa kuelekea mechi ya mwezi wa tatu, Yanga itaendelea kusimamisha minara.

Naye Katibu wa Tawi la Simba Dodoma, Salim Ali, amesema mwaka jana kwenye bonanza kama hili timu ya Simba iliibuka kinara katika michezo yote isipokuwa mpira wa miguu, na wamejipanga kuonyesha makali yao mwaka huu.

Mbunge na shabiki wa Simba, Magreth Sitta, amepongeza Azania Bank kwa udhamini wake na kusisitiza kuwa bonanza hilo litumike kuleta mshikamano, amani, na furaha miongoni mwa washiriki.

Mashabiki wote wanakaribishwa kushiriki bonanza hili la kipekee, ambalo linatarajiwa kuwa moja ya matukio makubwa ya michezo mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments

TAARIFA ZA WASTAAFU NHIF KUHAKIKIWA MAHALI WALIPO