CHONGOLO: ZANA ZA KILIMO NI UFUNGUO WA MUSTAKABALI WA KILIMO AFRIKA


📍Mkutano wa ACSAM waanzisha safari mpya ya kilimo cha kisasa Afrika

Na Asha Mwakyonde

WAZIRI wa Kilimo, Daniel Chongolo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwamini kuongoza Wizara hiyo katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo sekta ya kilimo imeainishwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu za kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Waziri Chongolo ametoa shukrani hizo wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, kufungua Mkutano wa kwanza wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization ACSAM), uliofanyika leo Februari 3, 2026 jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa mkutano huo umeleta pamoja viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kutoka ndani na nje ya Afrika kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha matumizi ya zana za kisasa katika kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.

Aidha, amewashukuru mawaziri wa kilimo kutoka nchi za Nigeria, Somalia, Niger, Afrika ya Kati, Rwanda na Senegal kwa kushiriki mkutano huo muhimu unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika maendeleo ya kilimo barani Afrika.

Waziri huyo ameongeza kuwa mkutano wa ACSAM umeanzishwa kama jukwaa la kipekee la kukutanisha watunga sera, wawakilishi wa serikali, wadau wa maendeleo, watafiti, wakulima, asasi za kiraia pamoja na sekta binafsi ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuendeleza matumizi ya zana za kilimo.

Kwa mujibu wa Waziri Chongolo, matumizi endelevu ya zana za kilimo ni hatua muhimu katika kuongeza tija mashambani, kuboresha kipato cha wakulima na kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo barani Afrika.

Amesisitiza kuwa kupitia mkutano huo, nchi za Afrika zina nafasi ya kujifunza na kuimarisha ushirikiano utakaosaidia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa bara zima.

Post a Comment

0 Comments

MAPINDUZI YA KIDIGITALI CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA YAMVUTIA WAZIRI HOMERA