MWIGULU: ZANA ENDELEVU ZA KILIMO NI NGUZO YA MAPINDUZI YA KILIMO AFRIKA


Na Asha Mwakyonde 

SERIKALI ya Tanzania imeeleza kuwa matumizi endelevu ya zana za kilimo ikiwa ni hatua muhimu katika kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula katika Bara la Afrika.

Kauli hiyo imetolewa leo Feburari 3,2026 jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba wakati akifungua rasmi Mkutano wa kwanza wa Kikanda wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (ACSAM) unaofanyika jijini Dar es Salaam. 

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Dk. Nchemba amesema kuwa Bara la Afrika kupitia Mfumo wa Zana Endelevu za Kilimo Barani Afrika (F-SAMA), Azimio la CAADP Kampala pamoja na Mkakati wa Miaka 10 wa CAADP (2026–2035) linaonesha dhamira ya pamoja ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kuvutia uwekezaji na kujenga mifumo himilivu ya chakula na lishe.

Amesema katika kutekeleza ajenda hiyo, Tanzania imeongeza uwekezaji katika huduma za zana za kilimo, kuendeleza ujuzi kwa vijana na kuimarisha taasisi za utafiti. Aidha, imeandaa Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo kwa kushirikiana na FAO, unaolenga kuimarisha matumizi na usimamizi endelevu wa teknolojia za kisasa katika mnyororo wa uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo.

Waziri Mkuu huyo ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuanzisha vituo jumuishi vya huduma za zana za kilimo nchini kote, ambapo itanunua matrekta 10,000 pamoja na zana zake ili kuanzisha vituo 1,000 katika ngazi ya kata. Hatua hiyo inalenga kuongeza tija katika uzalishaji, kupunguza gharama za kilimo na kuwapa wakulima nafasi ya kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo ili kuendeleza matumizi ya zana za kilimo.

Katika hatua nyingine, ametangaza kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kushirikiana na FAO katika mpango wa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Zana za Kilimo Barani Afrika, kabla ya kufungua rasmi mkutano huo na kuzindua Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili (2026–2035).

Post a Comment

0 Comments

MAPINDUZI YA KIDIGITALI CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA YAMVUTIA WAZIRI HOMERA