📍Mafanikio na mapungufu yawekwa wazi
Na Asha Mwakyonde, DODOMA
SEKTA ya maji nchini inaingia katika hatua mpya ya mageuzi inayochochewa na takwimu, uwajibikaji na shinikizo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na salama.
Pamoja na mafanikio yanayoanza kuonekana katika utoaji wa huduma, picha halisi inaonesha mchanganyiko wa mafanikio na changamoto zinazohitaji maamuzi ya haraka na ya kimkakati.
Katika muktadha huo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),imeweka wazi hali halisi ya utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/2025, taarifa inayobeba dira ya mafanikio, pamoja na tahadhari ya safari ndefu iliyosalia.
Pia sekta hiyo inaendelea kupiga hatua muhimu katika kuboresha huduma kwa wananchi, huku ikionesha mwelekeo mpya wa uwajibikaji, ufanisi na matumizi ya takwimu kwa kufanya maamuzi.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna pengo linalohitaji kuzibwa ili kufikia lengo la upatikanaji wa huduma bora, salama na endelevu kwa Watanzania wote.
Ripoti ya EWURA kupitia Muhtasari wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/25 inasema idadi ya watumishi katika mamlaka za maji imeongezeka kufikia 6,897 kutoka 6,837 mwaka uliopita, hatua inayochangia kuboresha uwiano wa watumishi kwa wateja.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa uwiano huo umeimarika hadi kufikia watumishi 3.7 kwa kila wateja 1,000, kutoka 4.0 mwaka 2023/24, hali inayokidhi viwango vinavyokubalika kitaifa.
Hata hivyo ripoti hiyo inafafanua kwamba maboresho hayo yameonekana pia kwa mamlaka nyingi zaidi kufikia kiwango hicho, ambapo mamlaka 50 zimekidhi vigezo hivyo ikilinganishwa na 24 mwaka uliopita.
HUDUMA KWA WATEJA
Aidha ripoti hiyo inaeleza kuwa mamlaka 73 sawa na asilimia 88 zimefanikiwa kuwa na mikataba ya huduma kwa wateja iliyoidhinishwa, hatua inayolenga kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Kwa mujibu wa ripoti ya EWURA, jumla ya malalamiko 463,740 yalipokelewa, ambapo asilimia 66 yalitatuliwa kikamilifu, ikilinganishwa na asilimia 61 mwaka uliopita.
“Kinachotia moyo zaidi ni kwamba asilimia 82 ya malalamiko yaliyotatuliwa yalishughulikiwa ndani ya siku tano za kazi, jambo linaloonesha kuimarika kwa mifumo ya huduma kwa wateja,” inasema ripoti hiyo.
Katika eneo la mipango na uwajibikaji, taarifa inaonesha kuwa mamlaka 53 kati ya 83 zina mipango ya biashara, huku mamlaka 81 zikiwa na programu za ufuatiliaji wa ubora wa majisafi na majitaka.
Uwasilishaji wa taarifa za kiutendaji na kifedha pia umeongezeka, hali inayochochea uwazi katika usimamizi wa sekta hiyo.
Hata hivyo, bado kuna changamoto katika maeneo kadhaa, ikiwemo baadhi ya mamlaka kushindwa kuwasilisha taarifa kwa wakati, ukosefu wa mipango ya biashara kwa baadhi ya taasisi, pamoja na ucheleweshaji wa tozo za udhibiti ambapo ni asilimia 47.46 tu ya makusanyo yaliyowasilishwa EWURA.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo utekelezaji wa maagizo ya ukaguzi umefikia asilimia 73, huku utekelezaji wa masharti ya bei za maji ukiongezeka hadi asilimia 64, ishara ya kuimarika kwa nidhamu ya kiutendaji katika mamlaka za maji.
Katika matokeo ya upimaji wa utendaji, mamlaka za maji za Moshi, Nzega na Biharamulo zimeibuka vinara katika makundi yao, zikionesha uwezo mkubwa wa utoaji huduma bora.
Hata hivyo, baadhi ya mamlaka zimeendelea kuonesha udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa malengo ya mipango ya biashara.
Aidha, uwepo wa Bodi za Wakurugenzi katika mamlaka 74 kati ya 83 umeelezwa kuwa ni chachu ya ufanisi, huku mamlaka tisa zisizokuwa na bodi zikitajwa kudhoofisha kasi ya maamuzi na usimamizi.
Kutokana na hali hiyo, EWURA imetoa mapendekezo mbalimbali kwa mamlaka za maji na Wizara ya Maji, yakiwemo kuboresha ubora wa maji, kuimarisha miundombinu ya majitaka, kupunguza upotevu wa maji, pamoja na kuongeza ushirikiano na sekta binafsi katika uwekezaji.
WIZARA YA MAJI
Kwa upande wa Wizara ya Maji, imehimizwa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji na majitaka, sambamba na kuhakikisha viwango vya ubora wa maji vinazingatiwa.
Kwa ujumla, tathmini hiyo imeonesha kuwa sekta ya maji inaendelea kuimarika, ingawa mafanikio hayo yanahitaji kuongezewa nguvu kupitia uwekezaji, ubunifu na usimamizi madhubuti.
“Ili kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya huduma bora za maji na usafi wa mazingira, ni lazima kuwe na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, EWURA, mamlaka za maji na wadau wote,” ilisisitiza ripoti hiyo ya EWURA.
Ripoti ya EWURA inaeleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa utakuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma, kuimarisha afya ya umma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
.jpg)
0 Comments