Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha usimamizi na ulinzi wa rasilimali za Taifa kwa kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo maalum yanayoendelea kufanyika.
Katika kufanikisha azma hiyo, Wizara imewakutanisha maofisa viungo kutoka wizara na taasisi za kisekta zinazosimamia rasilimali za nchi, na kuwapatia mafunzo ya siku nne yanayofanyika mjini Morogoro, yakilenga kuwajengea uwezo katika kusimamia na kulinda utajiri wa asili na maliasilia.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia, Bw. Everest Mashiba, alisema lengo kuu ni kuongeza weledi, uwajibikaji, uadilifu na ushirikiano miongoni mwa maofisa hao ili kuboresha usimamizi wa maliasili na kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, alibainisha kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kuimarisha uratibu wa taasisi mbalimbali. Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kusisitiza matumizi bora ya rasilimali za Taifa kwa kuzingatia tija, uwazi na kuhakikisha manufaa yake yanawanufaisha wananchi wote.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika mafunzo hayo ni usimamizi wa rasilimali za nchi, mifumo ya kisera na kisheria ya usimamizi wa hewa ukaa, pamoja na utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya uwekezaji.
Mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuimarisha weledi, ufanisi na ushirikiano miongoni mwa maofisa, ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wote na kuunga mkono malengo ya maendeleo endelevu, sambamba na kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2050.





0 Comments