MALIASILI NA UTALII WATATHMINI UTENDAJI WA ROBO TATU MWAKA DODOMA.


Na Anangisye Mwateba- Dodoma

WATAALAMU wa Ufuatiliaji na Tathimini wa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake wamekutana katika Kikao kazi cha Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kwa ajili ya Maandalizi ya Taarifa ya Ufuatiliaji na Utendaji Kazi wa Wizara kwa Kipindi cha Robo Tatu Mwaka (Julai, 2025 hadi Machi, 2026) katika Ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Bure Nassibu amesema kuwa lengo la kikao hicho ni Kujadili na Kuandaa Taarifa ya Ufuatiliaji wa Utendaji Kazi wa Wizara kwa kipindi cha Robo Tatu (Julai, 2025 – Machi, 2026) kwa kuzingatia viwango vya ubora na ushahidi wa utekelezaji.

Bi Bure aliongeza kuwa kikao hicho kinaongozwa na Kaulimbiu ya Kuimarisha Ufuatiliaji na Tathmini kwa Matokeo Endelevu ya Utekelezaji wa Sera, Mipango na Miradi ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026. Aidha, Wataalamu hao watafanya mapitio ya utekelezaji wa shughuli za Wizara ikiwemo kupima hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa shughuli dhidi ya malengo yaliyowekwa kwenye Mpango Kazi wa 2025/2026. 

Pia watachambua utekelezaji wa sera za Wizara Ikiwa ni pamoja na sekta za Wanyamapori, Misitu, Nyuki, Utalii na Mambo ya Kale. Vilevile watafuatilia maendeleo ya miradi na programu ili kubaini mafanikio, changamoto na hatua za kuboresha utekelezaji wake pamoja na kukusanya na kuainisha utekelezaji wa maelekezo ya viongozi (ngazi ya Wizara na Kitaifa) na kuhakikisha yanatekelezwa kikamilifu.

Kikao hicho kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Aprili, 2026 na kutoka na Taarifa ya Ufuatiliaji wa Utendaji Kazi wa Wizara kwa kipindi cha Robo Tatu Mwaka (Januari – Machi 2026) i inayozingatia miongozo ya Serikali ya Ufuatiliaji na Tathmini.



Post a Comment

0 Comments

MAPINDUZI SEKTA YA HAKI JINAI, SERIKALI YAIMARISHA MASHTAKA NA KUHARAKISHA HAKI