Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema sekta ya madini nchini inaendelea kuimarika kwa kasi, ikichangia kwa kiwango kikubwa mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi, kufuatia maboresho ya kimkakati yanayotekelezwa na Serikali.
Ameeleza hayo leo Aprili 27, 2026 wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini bungeni kwa mwaka wa fedha 2026/2027 amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ilipangiwa kukusanya maduhuli ya shilingi trilioni 1.41 kutoka vyanzo mbalimbali. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.20 zilitarajiwa kuwasilishwa Hazina na shilingi bilioni 205.54 kutumiwa na taasisi zilizo chini ya Wizara.
Amesema hadi kufikia Machi 2026, jumla ya shilingi trilioni 1.03 zimekusanywa na kuwasilishwa Hazina, sawa na asilimia 114.94 ya lengo la kipindi husika, mafanikio yanayoakisi kuimarika kwa mifumo ya ukusanyaji mapato.
Mavunde ameongeza kuwa Serikali imeimarisha usimamizi na ukaguzi katika maeneo ya uchimbaji, masoko ya madini, vituo vya ununuzi pamoja na mipaka ya nchi, hatua iliyosaidia kuongeza uwazi na kudhibiti upotevu wa mapato.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, biashara ya madini yenye thamani ya shilingi trilioni 4.90 imefanyika kupitia masoko na vituo vya ununuzi hadi Machi 2026, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.82 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, Mavunde amesema juhudi za kudhibiti utoroshaji wa madini zimeendelea kuimarika, ambapo kati ya Julai 2025 na Machi 2026, madini yenye thamani ya shilingi bilioni 3.31 yalikamatwa katika matukio 55 kwenye baadhi ya mikoa ya kimadini.
"Madini haya yalitaifishwa na Serikali na watuhumiwa wakichukuliwa hatua za kisheria," ameeleza Waziri huyo.
Aidha ametoa rai kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kulinda rasilimali za taifa na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya nchi.
Akizungumzia kuhusu mapato ya fedha za kigeni, Mavunde amesema mauzo ya madini nje ya nchi yameongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 5,401.9 mwaka 2025 kutoka dola milioni 4,119.9 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 31.1.
Amebainisha kuwa sekta ya madini ilichangia asilimia 52.57 ya mauzo yote ya bidhaa zilizouzwa nje mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 45.17 mwaka 2024. Pia, katika mauzo ya bidhaa zisizo za asili pekee, sekta hiyo ilichangia asilimia 63.73 mwaka 2025 kutoka asilimia 56.99 mwaka 2024.
Mavunde akizungumzia dhahabu, amesema thamani ya mauzo imeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 3,419.6 mwaka 2024 hadi dola milioni 4,753.9 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 39.0.
Akizungumzia mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa, Mavunde amesema umeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2023 hadi asilimia 10.1 mwaka 2024, huku hadi kufikia robo tatu ya mwaka 2025 ukifikia wastani wa asilimia 11.9, hali inayochangiwa na kuongezeka kwa uwekezaji.
Katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini muhimu na mkakati, Waziri huyo amesema Wizara kupitia Tume ya Madini imetoa leseni 454 kati ya Julai 2025 na Machi 2026, zikiwemo za madini ya kinywe, nickel, cobalt, lithium, heavy mineral sands na rare earth elements.
Amesisitiza kuwa utoaji wa leseni hizo unaweka msingi thabiti wa kukuza uwekezaji katika utafutaji na uendelezaji wa madini muhimu, hivyo kuongeza thamani ya rasilimali za taifa na kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.




0 Comments