TUME YA MADINI YAJIPANGA KUBORESHA LESENI NA KUDHIBITI UTOROSHWAAJI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imeweka mkakati kabambe wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, kuongeza mapato ya Serikali na kuhakikisha ushiriki mpana wa Watanzania katika Mwaka wa Fedha 2026/2027, hatua inayotarajiwa kuleta tija zaidi katika uchumi wa nchi.

Akiwasilisha leo Aprili 27,2026 bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Tume ya Madini itaendelea kutoa na kufuatilia leseni za shughuli mbalimbali za madini, sambamba na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Madini.

Ameeleza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wamiliki wa leseni watakaokiuka masharti, ikiwemo kusimamishwa au kufutiwa leseni zao.

Amesema Tume itaendelea kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo na kuongeza mchango wao katika pato la taifa.

Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, Mavunde ameeleza kuwa Tume ya Madini itahakikisha migodi mikubwa na ya kati inaanza uzalishaji kwa wakati, pamoja na kusimamia kwa karibu masoko ya madini na vituo vya ununuzi ili kudhibiti vitendo vya utoroshwaji wa madini.

Aidha, juhudi zitaelekezwa katika kupanua wigo wa usimamizi kwenye madini ya ujenzi na ya viwandani, pamoja na kufanya tafiti za kubaini vyanzo vipya vya mapato.

Kwa upande wa usalama na mazingira, Waziri Mavunde amesema Tume itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika migodi midogo, ya kati na mikubwa ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia viwango vya afya, usalama na utunzaji wa mazingira. Ukaguzi huo utahusisha pia maeneo hatarishi kama mabwawa ya topetaka (TSF), sehemu za kuhifadhia miambataka na maghala ya baruti.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya uendelezaji na ufungaji wa migodi, huku ikichukua hatua stahiki kuhakikisha wachimbaji wanafuata taratibu salama ili kuepusha ajali zisizo za lazima.

Kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania, Mavunde amesema Tume ya Madini itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera ya Local Content, kwa kuhakikisha kampuni za madini zinanunua bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi. Aidha, orodha ya huduma na bidhaa zinazopaswa kutolewa na Watanzania kwa asilimia 100 itaendelea kutangazwa na kusimamiwa ipasavyo.

Amesisitiza kuwa ni marufuku kwa mtu asiye Mtanzania kushiriki katika utoaji wa huduma au usambazaji wa bidhaa zilizotengwa kwa wazawa pekee, huku pia kampuni za madini zikihimizwa kutekeleza wajibu wao kwa jamii (CSR) kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo.

Katika kuboresha utendaji kazi wa Tume, Waziri huyo amesema mipango imewekwa ya kuboresha miundombinu na rasilimali watu, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa ofisi za Afisa Madini katika maeneo mbalimbali nchini. Pia, ununuzi wa vitendea kazi kama magari, pikipiki, kompyuta, vifaa vya ukaguzi na masoko ya madini utafanyika ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Aidha, Tume itawekeza katika maendeleo ya watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika kada mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza weledi na ufanisi katika usimamizi wa sekta ya madini.

Hatua hizi zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuifanya sekta ya madini kuwa mhimili imara wa uchumi, wenye manufaa kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla.
 

Post a Comment

0 Comments

TUME YA MADINI YAJIPANGA KUBORESHA LESENI NA KUDHIBITI UTOROSHWAAJI