Na Asha Mwakyonde, TANGA
WAKATI Tanzania ikiendelea kusukuma ajenda ya ubunifu na matumizi ya teknolojia zinazozalishwa ndani ya nchi, Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Pwani kimeanza hatua muhimu ya kutengeneza simu kwa kutumia teknolojia yake yenyewe ambayo inayojulikana kama 'Ujuzi Pro 0S' ikiwa ni sehemu ya utafiti unaolenga kuzalisha simu zinazoweza kushindana na zile zinazotumika kwa sasa.
Ubunifu huo unaoendelea katika VETA unalenga kutengeneza simu kuanzia hatua za awali kwa kutumia teknolojia iliyobuniwa na watafiti wa ndani, badala ya kutegemea mifumo iliyotengenezwa na wazalishaji wa nje.
Akizungumza katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, kuhusu utafiti huo,
Mkufunzi wa VETA Pwani, Hamis Salum, ambaye ni miongoni mwa wataalamu wakuu wanaoshiriki katika utafiti huo, amesema timu hiyo tayari imefanikiwa kutengeneza simu inayoweza kufanya kazi mbili za msingi, ambazo ni kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (SMS).
Amesema mafanikio hayo ni hatua ya mwanzo katika safari ya kutengeneza simu yenye uwezo mpana zaidi, huku akieleza kuwa utafiti huo umefikia mwaka wa pili na bado unaendelea.
“Kwa sasa tumefikia hatua ambayo simu inaweza kupiga simu na kutuma SMS, ambazo ndizo kazi za msingi kabisa za simu. Pia simu hii inaweza kubebeka,” amesema Salum.
Kwa mujibu wa Salum, moja ya mambo muhimu katika ubunifu huo ni matumizi ya motherboard iliyotengenezwa na timu yenyewe, hatua inayodhihirisha jitihada za VETA kujenga uwezo wa ndani katika kubuni na kutengeneza teknolojia.
Mkufunzi huyo ameeleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna kazi kubwa ya kukamilisha kabla ya simu hiyo kufikia kiwango kinacholengwa na watafiti, ikiwemo kuongeza uwezo wa kufanya kazi mbalimbali na kupunguza ukubwa wake.
“Utafiti huu bado unaendelea kwa sababu haujafikia malengo yake. Tunataka simu hii iwe na uwezo unaopatikana kwenye simu tunazotumia sasa, lakini kwa sasa ina uwezo wa kupiga simu na kutuma SMS pekee,” amesema.
Ameongeza kuwa timu hiyo inalenga kuboresha muundo wa simu hiyo ili iwe ndogo na nyepesi zaidi, sawa na simu za kisasa zinazotumika kwa sasa, badala ya kuwa na ukubwa ilionao katika hatua hii ya utafiti.
Salum amesema hatua iliyofikiwa inaonyesha kuwa wataalamu wa ndani wana uwezo wa kubuni teknolojia kutoka hatua za awali na kwamba utafiti huo ukikamilika unaweza kuwa sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji wa vifaa vya kiteknolojia nchini.
Utafiti huo unaendelea huku wataalamu wa VETA wakilenga kuongeza uwezo wa simu hiyo, kuboresha ukubwa na muundo wake pamoja na kuifikisha katika hatua ambayo itaweza kutoa huduma nyingi zaidi kama zilivyo kwenye simu za kisasa.



0 Comments