MWANAFUNZI UDOM ABUNI MFUMO KUREJESHA SIMU ZILIZOPOTEA

Na Asha Mwakyonde, TANGA

TEKNOLOJIA imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto ya upotevu na wizi wa simu, huku mfumo wa kisasa ukitoa fursa kwa watumiaji kufuatilia mahali kifaa kilipo na kuongeza uwezekano wa kukirejesha.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Kozi ya Uhandisi wa Kompyuta kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Emmanuel Mpyambala,amebuni mfumo unaoitwa 'VexGuard Anti-Theft System' ambao unaolenga kusaidia katika ufuatiliaji wa simu zilizopotea au kuibwa.

Akizungumza katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akielezea namna teknolojia hiyo inavyoweza kutumika, Mpyambala amesema mtu aliyepoteza simu anaweza kutumia kifaa kingine, ikiwemo simu ya rafiki au ndugu, kupakua programu ya ufuatiliaji wa vifaa kupitia Play Store na kuingia kwa kutumia akaunti iliyokuwa imeunganishwa na simu iliyopotea.

Amesema baada ya kuingia katika akaunti hiyo, mtumiaji anaweza kuona vifaa vilivyounganishwa na akaunti na kuchagua simu iliyopotea ili kupata taarifa kuhusu eneo ilipo kupitia mfumo wa GPS.

“Mtumiaji anaweza kuona location ya simu yake, kuifunga ili isiweze kutumiwa na mtu mwingine na kuchukua hatua nyingine za usalama,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya mifumo ya kisasa inaruhusu mtumiaji kuweka ujumbe au taarifa za mawasiliano kwenye simu iliyopotea, hatua inayoweza kumwezesha mtu aliyeikuta kuwasiliana na mwenye kifaa hicho.

Hata hivyo, amesema endapo simu imeibwa au mtumiaji ameshindwa kuipata, ni muhimu kutoa taarifa kwa Polisi ili uchunguzi ufanyike kwa kuzingatia taratibu na sheria.

Amesema taarifa kuhusu eneo la kifaa zinaweza kuwa muhimu katika uchunguzi, huku Polisi wakitumia taratibu zinazohitajika pamoja na teknolojia zinazopatikana kisheria katika kufuatilia kifaa na kubaini mahali kinapoweza kuwa.

Kwa mujibu wa Mpyambala, matumizi sahihi ya teknolojia pamoja na ushirikiano kati ya wananchi, Polisi na sekta mbalimbali yanaweza kusaidia kupunguza matukio ya wizi wa simu, kwa kuwa vifaa vilivyoibwa vinaweza kufuatiliwa na kubainika vilipo.

Post a Comment

0 Comments

VETA YAANZA KUUNDA SIMU ZA KITEKNOLOJIA YA NDANI