Na Asha Mwakyonde, TANGA
WAKULIMA wanaweza kupunguza hasara inayotokana na kuharibika kwa mazao yaliyohifadhiwa maghalani baada ya Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jospeter Kaizelege, kubuni mfumo wa GT-95 unaofuatilia mazingira ya uhifadhi wa mazao na kutoa taarifa muhimu kwa wakati.
Kaizelege, ambaye pia ni mwanzilishi wa kampuni ya Maxwell Track Ghala, amesema mfumo huo umebuniwa kutokana na changamoto wanazokutana nazo wakulima baada ya kuvuna mazao na kuyahifadhi kabla ya kuyapeleka sokoni.
Akizungumza katikaka Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu amesema moja ya changamoto kubwa ni mabadiliko ya kiwango cha unyevu nyevu na joto katika maeneo ya kuhifadhia mazao, hali inayoweza kusababisha mazao kupata ukungu, kuvamiwa na wadudu na hatimaye kuharibika.
Kwa mujibu wa Kaizelege, mkulima anaweza kuhifadhi mazao kwa muda akitarajia kuyauza baada ya miezi kadhaa, ambapo anapofika wakati wa kuuza anaweza kukuta sehemu ya mazao imeharibika kutokana na mazingira yasiyofaa ya uhifadhi.
Amesema kabla ya mfumo huo, wakulima walilazimika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa njia za kawaida ili kubaini kama mazao yameanza kupata ukungu, wadudu wameingia au unyevu umeongezeka.
“Tunachofanya ni kumsaidia mkulima kupata taarifa za hali ya mazao yake kwa wakati. Mfumo unaweza kufuatilia mambo kama unyevu na joto, hivyo mkulima anaweza kujua mapema kama mazingira ya ghala yanaweza kusababisha uharibifu,” amesema Kaizelege.
Amesema mfumo wa GT-95 unalenga kupunguza utegemezi wa ukaguzi wa macho pekee, kwa kuwezesha ufuatiliaji wa mazingira ya ghala na kutoa taarifa zinazoweza kumsaidia mhifadhi kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.
Kaizelege amesema tayari wameanza kufanya kazi na baadhi ya watumiaji wa mfumo huo na wameanza kupata matokeo mazuri, huku kampuni yake ikiendelea kuutangaza na kuwafikia watumiaji zaidi.
“Tumeanza kufanya kazi na baadhi ya watumiaji na kifaa kinawapa matokeo mazuri. Tunaendelea pia kukitangaza hapa Tanga,” amesema.
Ameongeza kuwa katika mkoani Dodoma, wameanza kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), katika jitihada za kutumia teknolojia hiyo kuboresha uhifadhi wa mazao.
Kwa mujibu wa Kaizelege, lengo kubwa la ubunifu huo ni kusaidia kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza ufanisi katika uhifadhi na kumwezesha mkulima kupata thamani zaidi ya mazao yake wakati wa kuyafikisha sokoni.
Amesema matumizi ya teknolojia katika uhifadhi wa mazao ni muhimu katika kuhakikisha mazao hayapotei kabla ya kuuzwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuwapa wakulima na wahifadhi mifumo inayowawezesha kupata taarifa sahihi na kuchukua hatua kwa wakati.
Ubunifu wa GT-95 unaonyesha namna wataalamu kutoka vyuo vikuu nchini wanavyotumia maarifa na teknolojia kutengeneza suluhisho zinazolenga kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima na sekta ya kilimo kwa ujumla.

0 Comments