Na Asha Mwakyonde, TANGA
TANZANIA imeweka mkazo katika kuimarisha elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu ili kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, kupunguza utegemezi wa teknolojia na wataalamu kutoka nje ya nchi, pamoja na kuongeza kasi ya uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazotokana na maarifa ya Watanzania.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu katika kujenga Taifa lenye uwezo wa kutengeneza suluhisho zake kwa changamoto zinazolikabili, huku Serikali ikisisitiza kuwa uwekezaji katika utafiti na ubunifu unapaswa kuzaa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi na uchumi wa Taifa.
Hayo yameswmwa leo Agosti 18, 2026, na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizindua Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Usagara, ambapo pia aliwatunuku tuzo watafiti 154 waliofanya vizuri katika tafiti zilizochapishwa kwenye majarida ya kimataifa.
Prof. Mkenda amesema Tanzania ina wataalamu wenye uwezo mkubwa, hivyo Serikali ina wajibu wa kuendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha kutumia maarifa yao kubuni bidhaa, huduma na teknolojia zinazokidhi mahitaji ya ndani na kuwa na ushindani katika masoko ya kimataifa.
Amesema uwekezaji katika elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu ni sehemu muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea kujitegemea zaidi, kwa kuwa Taifa haliwezi kuwa na uchumi imara bila kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuzalisha maarifa na kuyageuza kuwa suluhisho.
“Serikali inatoa ufadhili wa asilimia 100 kwa lengo la kujenga sayansi na teknolojia nchini,” amesema Prof. Mkenda.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika taasisi za elimu na mafunzo ya sayansi, teknolojia na ujuzi, sambamba na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya uchumi wa kisasa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, utafiti na ubunifu vinapaswa kuelekezwa zaidi katika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, afya, uzalishaji na mazingira.
Prof. amesisitiza pia umuhimu wa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira na zinazozingatia mahitaji ya kizazi cha sasa bila kuhatarisha uwezo wa kizazi kijacho kukidhi mahitaji yake.
WATAFITI 154 WATUNUKIWA
Katika hafla hiyo, Prof. Mkenda amewatunuku tuzo watafiti 154 waliobobea katika tafiti zilizochapishwa kwenye majarida ya kimataifa, hatua ambayo amesema inalenga kutambua na kuhamasisha wataalamu kuendelea kufanya tafiti zenye ubora na mchango kwa maendeleo ya Taifa.
Washindi hao wametoka katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma, yakiwemo sayansi asilia, afya na sayansi shirikishi, sayansi ya kilimo na wanyama, pamoja na sayansi ya uhandisi na TEHAMA.Washindi walipatiwa vyeti pamoja na zawadi za fedha zenye jumla ya Sh milioni 50.
Prof. Mkenda ameeleza utambuzi huo ni sehemu ya kuhamasisha watafiti na wabunifu kuendelea kutumia ujuzi na maarifa yao katika kutengeneza suluhisho zitakazosaidia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali na kuongeza ushindani wake kimataifa.
SERIKALI YAONGEZA FURSA KWA VIJANA
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji katika ubunifu kushiriki mashindano ya kimataifa, hatua ambayo itawawezesha kupima uwezo wao dhidi ya vijana kutoka mataifa mengine na kujenga uzoefu katika teknolojia na ubunifu.
Amesema Serikali pia imeendelea kujenga shule za sayansi katika mikoa mbalimbali na kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye vipaji, ikiwa ni mkakati wa kuongeza idadi ya wataalamu katika maeneo ya sayansi na teknolojia.
Waziri huyo ameeleza kuwa maboresho yanayoendelea kufanyika katika sekta ya elimu, ikiwemo sera na mitaala, yanalenga kuifanya elimu kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii na kuwaandaa vijana wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika dunia ya sasa.
Kwa upande mwingine, amezitaka taasisi za elimu, watafiti, wabunifu, vijana na wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kujenga Tanzania inayojitegemea kupitia elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utasaidia Taifa kuongeza uzalishaji wa wataalamu, bidhaa na teknolojia zenye uwezo wa kushindana ndani na nje ya nchi, huku ukitoa nafasi kwa maarifa yanayozalishwa nchini kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za wananchi.
Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 inaendelea jijini Tanga ikiwa ni jukwaa la kuonesha mafanikio, tafiti, bunifu na fursa mbalimbali katika sekta ya elimu, ujuzi, sayansi na teknolojia. ujumbe wake mkuu ukiwa ni kuhamasisha matumizi ya maarifa na ubunifu katika kujenga maendeleo endelevu ya Taifa.





0 Comments