PROF. KONDORO: COSTECH YALENGA KUZALISHA UBUNIFU WENYE TIJA


Na Asha Mwakyonde, TANGA 

WAKATI mawazo ya ubunifu yakiongezeka miongoni mwa vijana nchini, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),imeelekeza nguvu katika kuyapa mawazo hayo njia ya kufikia utekelezaji na soko huku ikisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wabunifu kupata ujuzi na mitaji ya kuendeleza bidhaa zao.

COSTECH itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kukuza ubunifu wa vijana na kuhakikisha bunifu zao zinapata fursa ya kufikia soko na kutatua changamoto za jamii.

Akizungumza leo Agosti 18,2026 kwenye banda la Tume hiyo katika Maonesho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika jijini Tanga Mwenyekiti wa Bodi ya COSTECH, Profesa John Kondoro amesema wanashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na vyuo vya elimu ya juu kama Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (DIT), Arusha Technical College na taasisi nyingine lengo likiwa ni kuwasaidia wabunifu kuboresha bidhaa zao na kuzifikisha sokoni.

Amesema COSTECH imejikita katika kuchochea ubunifu kupitia mashindano, maonesho na uwezeshaji wa wabunifu.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa maonesho hayo yamekuwa fursa kwa COSTECH kuonesha bunifu mbalimbali huku pia yakitoa nafasi kwa wananchi kutambua uwezo uliopo miongoni mwa vijana na watafiti katika kutengeneza bidhaa na teknolojia zinazoweza kutumika katika jamii.

“Tupo hapa kuchochea ubunifu mbalimbali ili uweze kuendelezwa. Pia tuko tayari kusaidia na kuwezesha kifedha ili bunifu hizo ziweze kufika sokoni,” amesema Prof  Kondoro.

Amesema pamoja na kuonesha bunifu, COSTECH inatumia mashindano ya kitaifa ya ubunifu na maarifa kama sehemu ya kuwahamasisha vijana kuongeza uwezo wao wa kufikiri, kubuni na kutengeneza suluhisho zenye tija.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unalenga kuwapa wabunifu mazingira bora ya kuboresha ujuzi wao kutoka hatua ya kuwa na wazo hadi kutengeneza bidhaa inayoweza kushindana na kukubalika katika soko.

“Tunafanya kazi pamoja na VETA na taasisi za elimu ya juu. Mtu mwenye ubunifu anaweza kwenda katika taasisi hizi ili kuboresha zaidi uwezo wake na kufikia kiwango cha kuingia sokoni,” amesema.

Amesisitiza kuwa changamoto kubwa si kuwa na wazo pekee, bali ni namna mbunifu anavyoweza kuliboresha, kulifanya kuwa bidhaa au huduma yenye ubora na hatimaye kulifikisha kwa watumiaji.

Kwa mujibu wa Prof. Kondoro, COSTECH itaendelea kutoa usaidizi na kuwezesha wabunifu ili mawazo yao yasibaki kwenye maonesho pekee, bali yaende hatua zaidi na kuwa bidhaa na huduma zinazoweza kuchangia maendeleo ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments

VETA YAANZA KUUNDA SIMU ZA KITEKNOLOJIA YA NDANI