Na Asha Mwakyonde, TANGA
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kimeendelea kuimarisha nafasi yake katika utafiti na uzalishaji wa maarifa, baada ya watafiti wake zaidi ya 14 kutambuliwa na kutunukiwa tuzo kwa machapisho yao yaliyochapishwa katika majarida ya kimataifa yenye viwango na kutambulika katika mifumo ya kimataifa ya utafiti.
Tuzo hizo zimetolewa leo Agosti 18 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kutambua na kuhamasisha watafiti wanaochangia katika uzalishaji wa maarifa na utatuzi wa changamoto za jamii.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM anayeshughulikia masuala ya Utafiti, Profesa Nelson Boniface, amesema chuo hicho kinajivunia mafanikio yanayoendelea kupatikana katika tafiti na machapisho ya kitaaluma yanayozalishwa na watafiti wake.
Prof. Boniface amesema asilimia 52 ya machapisho ya watafiti wa UDSM yanachapishwa katika majarida ya kimataifa yenye viwango vya juu, yakiwemo majarida yaliyo katika kundi la Q1, pamoja na yale yanayotambuliwa katika mifumo ya Web of Science na Scopus.
Ameelza kuwa baadhi ya tafiti na machapisho hayo pia huchapishwa kupitia wachapishaji wakubwa wa kimataifa, akitolea mfano kampuni ya Elsevier, jambo linaloonyesha kiwango cha ubora wa tafiti zinazozalishwa na watafiti wa chuo hicho.
Kwa mujibu wa Prof. Boniface, ukuaji wa machapisho katika majarida hayo umefikia asilimia 16, hali ambayo amesema ni ishara ya kuongezeka kwa ubora, tija na ushindani wa tafiti zinazofanywa na UDSM katika ngazi ya kimataifa.
Ameongeza kuwa watafiti waliotambuliwa kupitia tuzo hizo wamefanya tafiti katika maeneo mbalimbali yenye umuhimu kwa maendeleo ya jamii, yakiwemo afya, sayansi asilia kama hisabati na fizikia, pamoja na uhandisi.
Prof. Boniface ameeleza kuwa tafiti hizo zinalenga kuongeza maarifa na, wakati huo huo, kutafuta majawabu ya changamoto zinazozikabili jamii na sekta mbalimbali, hivyo kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi.
“Kutambuliwa kwa watafiti hawa ni ishara ya mchango unaotolewa na UDSM katika uzalishaji wa maarifa kupitia tafiti zenye viwango vya kimataifa,” amesema Prof. Boniface.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya UDSM katika kufanya tafiti zenye ubora na kuzalisha machapisho yanayoweza kutumika katika kutatua changamoto za maendeleo, hususan katika nyanja za afya, sayansi asilia, biolojia na uhandisi.
Ameongeza kuwa kutambuliwa kwa watafiti hao kupitia tuzo hizo kunatoa motisha kwa watafiti wengine kuendelea kufanya tafiti zenye ubora na kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanafikia jamii na kuchangia ka
tika maendeleo ya Taifa.

0 Comments