VIJANA WAPEWA JUKUMU LA KUENEZA ELIMU YA KISHERIA NCHINI


 Na Mwandishi wetu, DODOMA 

SERIKALI imeendelea kuyafikia makundi mbalimbali wakiwemo vijana kufuatia ushiriki wao katika mdahalo uliolenga kujadili namna wanavyoweza kuchochea upatikanaji wa huduma za kisheria, kutambua haki, wajibu na upatikanaji wa huduma za Msaada wa Kisheria kwa wananchi bila malipo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi,wakati wa mdahalo uliowakutanisha wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Mawakili wa Serikali, wataalam wa TEHAMA na Wataalam wa masuala ya kijamii.

“Tunataka vijana wapate uelewa wa kutosha juu ya masuala ya kisheria ili waweze kufahamu namna bora ya kuweza kufanya pindi wanapokutana na mambo yanayohitaji Msaada wa Kisheria.Aidha, kuhakikisha tunapata mabalozi wazuri wa elimu ya kisheria kwa jamii zinazowazunguka.Alisema Msambazi.

Katika hatua nyingine, Amidi wa Shule Kuu ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Elia Mwanga, amesema kuwa ushiriki wa vijana ni hatua muhimu katika kuleta uelewa wa pamoja na kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.Alibainisha kuwa kupitia majukwaa ya elimu,mitandao ya kijamii na shughuli za kijamii vijana wanapata fursa ya kutoa maoni yao yatakayowezesha kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya kisheria katika maeneo mbalimbali kutokana na jiografia ya maeneo wanapotoka.

Wakizungumza katika nyakati tofauti tofauti baadhi ya vijana walioshiri kutoka chuoni hapo wamepongeza kuanzishwa kwa jukwaa hilo, wakisema limewapa mwanga kuhusu masuala ya kisheria sambamba na upatikanaji haki.

Wizara imeendelea kutumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha elimu ya kisheria inaifikia jamii ikiwa ni pamoja na majukwa ya elimu yatakayowezesha vijana kuwa mabalozi wa haki,yakihimiza matumizi ya teknolojia na mbinu bunifu katika kufikisha elimu ya kisheria kwa wananchi.







Post a Comment

0 Comments

KAGERA KUNUFAIKA NA MPANGO WA MKOA WA AFYA MOJA