SERIKALI YAONGEZA NGUVU KUJENGA WATAALAM WA SHERIA, HUDUMA KUSOGEZWA KARIBU NA WANANCHI

Na Asha Mwakyonde, DODOMA 

SERIKALI imeongeza nguvu katika kuendeleza rasilimali watu ndani ya sekta ya sheria, ikilenga kujenga mfumo imara wa utoaji haki unaozingatia weledi, uwazi na ufanisi kwa manufaa ya wananchi wote.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Juma Homera ameeleza hayo  leo Aprili 24, 2026 bungeni wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, akibainisha kuwa wizara inatambua rasilimali watu kuwa mhimili mkuu wa utoaji wa huduma bora za kisheria nchini.

Amesema Wizara pamoja na taasisi zake imeendelea kuajiri na kuendeleza watumishi kwa kuwajengea uwezo kupitia mafunzo ya ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha utendaji kazi wa sekta ya sheria.

Dk. Homera amesema maboresho makubwa yamefanyika katika Miundo ya Maendeleo ya Utumishi, ambapo kada zimeongezeka kutoka moja hadi kufikia kada 11.

 Kada hizo ni pamoja na Mawakili wa Serikali, Maafisa Sheria, Waandishi wa Sheria, Makatibu Sheria, Maafisa Uchunguzi, Maafisa Usajili na kada nyingine saidizi.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Kada ya Wasaidizi wa Sheria kutawawezesha watumishi hao kufika hadi ngazi ya vijiji, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa huduma za kisheria na kusogeza haki karibu zaidi na wananchi.

Akizungumzia hali ya watumishi, amesema Wizara ina jumla ya watumishi 643, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 imeajiri watumishi 45, imethibitisha kazini watumishi 449, imepandisha vyeo watumishi sita na kuwateua watumishi watatu katika nafasi za uongozi.

Ameongeza kuwa watumishi 10 wamehamia kutoka taasisi mbalimbali huku 21 wakihamia taasisi nyingine, hali inayoonyesha mzunguko wa kitaaluma ndani ya utumishi wa umma.

Kuhusu mafunzo, Dk.Homera amesema watumishi 32 wamewezeshwa kupata mafunzo ya muda mrefu katika maeneo ya kimkakati ikiwemo utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, mafunzo ya vitendo ya uanasheria, haki za binadamu na sheria zinazohusiana na teknolojia ya akili unde.

Aidha, watumishi 56 wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi, ambapo 31 walipata mafunzo ndani ya nchi na 25 nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ujuzi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu utaendelea kuwa kipaumbele cha wizara ili kuhakikisha sekta ya sheria inakuwa na wataalam wenye uwezo wa kutoa huduma bora na kusaidia wananchi kupata haki kwa wakati na kwa usawa.

Post a Comment

0 Comments

VIPAUMBELE 17 KULETA MAGEUZI SEKTA YA SHERIA