Na Asha Mwakyonde, DODOMA
JUHUDI za Serikali za kusambaza nishati safi na ya uhakika vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) zimeendelea kuonesha matokeo chanya katika uhifadhi wa mazingira, huku miradi mbalimbali inayotekelezwa ikitajwa kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamebainishwa leo Juni 5, 2026, na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, alipotembelea banda la REA katika kilele cha Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo, Balozi Dkt. Nchimbi alipata maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati inayotekelezwa na Wakala huo katika maeneo ya vijijini kutoka kwa Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage.
Mhandisi Mwijage amesema kuwa REA imeendelea kutekeleza miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi na salama kwa wananchi wa vijijini, hatua ambayo imechangia kupunguza matumizi ya nishati zinazochochea uharibifu wa mazingira.
Ameeleza kuwa miradi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati jadidifu ambazo ni rafiki kwa mazingira.
Maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2026 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania,” inayosisitiza umuhimu wa ushiriki wa wadau wote katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

0 Comments