Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ameipongeza Taasisi ya Inades Formation Tanzania (IFTz) kwa juhudi zake za kuhifadhi mbegu za asili, kuhamasisha upandaji miti na kuendeleza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira zinazosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.
Masauni ametoa pongezi hizo leo Juni 4,2026 alipokuwa akitembelea banda la taasisi hiyo katika wiki ya mazingira yalioenda sambamba na Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma, ambapo ameeleza kuridhishwa na kazi zinazotekelezwa na shirika hilo katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.
Amesema INADES imeonyesha dhamira ya dhati ya kushiriki juhudi za Taifa za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi mbalimbali inayolenga uhifadhi wa mazingira na kuongeza ustahimilivu wa jamii.
Akitoa maelezo kuhusu shughuli za taasisi hiyo, Afisa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka INADES, Adaisy Mola, amesema shirika hilo linaendesha programu mbalimbali za mafunzo kwa njia ya masafa pamoja na miradi ya mazingira inayolenga kuhifadhi maarifa na teknolojia za asili zinazotokana na jamii.
Amesema miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni ule wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika wilaya za Chemba na Bahi mkoani Dodoma, ambapo taasisi hiyo imeweka mkazo katika uhifadhi wa mbegu za asili ambazo ziko katika hatari ya kutoweka.
“Tunatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo uhifadhi wa mbegu za asili kwa kuwa baadhi yake zipo kwenye hatari ya kupotea. Hii ni sehemu ya jitihada za kulinda urithi wa kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula kwa vizazi vijavyo,” amesema Mola.
Mola ameongeza kuwa mwezi Januari mwaka huu taasisi hiyo ilizindua kampeni ya upandaji miti ijulikanayo kama ‘Tilinda Kesho Yetu’, yenye lengo la kuzalisha na kupanda miti milioni moja ifikapo mwaka 2028.
Kwa mujibu wa Mola, hadi sasa miti 15,000 imepandwa katika Wilaya ya Bahi, miti 1,170 katika Wilaya ya Chemba na miti 3,357 katika Wilaya ya Kondoa, ambapo miti hiyo inapandwa katika taasisi mbalimbali pamoja na mashamba ya wakulima.
Aidha, ameeleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikihamasisha matumizi ya mzinga wa nyuki wa udongo, teknolojia inayosaidia kupunguza ukataji wa miti unaotokana na matumizi ya mizinga ya kawaida inayohitaji mbao nyingi.
Mbali na hilo, amesema INADES inaendesha programu za mafunzo katika maeneo ya uongozi na maendeleo, pamoja na kilimo, ufugaji na uhifadhi wa mazingira kupitia machapisho na vitabu vinavyotumiwa kuwajengea uwezo wananchi.
Amebainisha kuwa taasisi hiyo inatekeleza miradi kwa ufadhili wa mashirika mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la Ujerumani pamoja na mradi wa ustawi wa punda unaotekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ufadhiliwa Brooke East Africa.
Kwa upande wake, mkulima mnufaika wa miradi ya INADES kutoka Kondoa DC, Christina Frank, amesema jamii nyingi za vijijini zimeanzisha benki za mbegu za asili kwa lengo la kuzihifadhi na kuzirejesha katika matumizi baada ya baadhi yake kuanza kutoweka kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mbegu za kisasa.
“Nimekuja katika maonesho haya kuonesha umuhimu wa mbegu za asili kwa sababu kwa sasa watu wengi wamejikita zaidi katika matumizi ya mbegu za kisasa,” amesema.
Naye Raphael Mungia kutoka Kijiji cha Isini, Kata ya Paranga, Wilaya ya Chemba, amesema wakulima katika eneo hilo wanatumia teknolojia ya kipima mvua cha asili kinachowasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu muda na aina ya mazao ya kupanda.
Amesema teknolojia hiyo humwezesha mkulima kufahamu kiwango halisi cha mvua kilichonyesha kabla ya kuanza shughuli za upandaji, jambo linalosaidia kupunguza hasara zinazoweza kujitokeza pale mvua zinapokatika ghafla baada ya kupanda.
“Kwa kutumia kipimo hiki mkulima anaweza kujua mvua imenyesha kwa kiwango gani na kuamua aina ya zao linalofaa kupandwa kulingana na unyevu uliopo ardhini,” amesema.



0 Comments