UDSM YABUNI MFUMO WA KUPIMA NGUO KABLA YA KUNUNUA


 Na Asha Mwakyonde, TANGA

WAKATI ununuzi wa nguo mtandaoni ukiendelea kukua, changamoto ya kujua kama vazi linakutosha kabla ya kulinunua imekuwa kikwazo kwa baadhi ya wateja. Ili kuondoa usumbufu huo, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kelvin Erasto, amebuni mfumo unaolenga kumwezesha mtu kuchagua na kupima nguo akiwa nyumbani bila kulazimika kwenda dukani.

Erasto, mwanafunzi wa mwaka wa nne anayesoma Computer Engineering and Information Technology katika UDSM, amesema mfumo huo umeundwa kurahisisha mchakato wa ununuzi wa nguo kwa kuwaunganisha watumiaji na maduka mbalimbali yanayouza mavazi.

Amesema kupitia mfumo huo, mtumiaji anaweza kutazama nguo zinazopatikana katika maduka yaliyoshirikishwa na kufanya mchakato wa kuchagua vazi akiwa nyumbani, hatua inayolenga kupunguza muda na usumbufu wa kwenda dukani, kupima nguo na kurejea tena nyumbani.

“Ni rahisi kwa sababu badala ya kwenda dukani, kupima nguo na kurudi nyumbani, unaweza kufanya michakato hiyo ukiwa nyumbani,” amesema Erasto.

Ameeleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na maduka mbalimbali, hivyo mtumiaji anapoingia katika mfumo anaweza kuona bidhaa za mavazi kutoka kwa wafanyabiashara hao na kufanya uchaguzi kulingana na mahitaji yake.

Hata hivyo, amesema mfumo huo bado uko katika hatua za maboresho, huku timu yake ikiendelea kurekebisha changamoto zinazojitokeza ili kuongeza ufanisi na kufanya mfumo huo kuwa rafiki zaidi kwa watumiaji.

“Bado kuna makosa hapa na pale, lakini tunaendelea kuyarekebisha na kuboresha mfumo zaidi ili watu waweze kuupenda na kuutumia kwa urahisi,” amesema.

Kwa mujibu wa Erasto, ubunifu huo pia unalenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wabunifu wanaojihusisha na mavazi kupata fursa ya kutangaza na kukuza biashara zao kupitia teknolojia.

Amesema wapo watu wengi wenye mawazo na biashara zinazohusiana na mavazi na mitindo, lakini baadhi yao bado hawajapata nafasi kubwa ya kukuza biashara zao, hivyo mfumo huo unalenga kuwawezesha kutumia teknolojia kufikia wateja wengi zaidi.

“Lengo letu ni kuwawezesha wale ambao bado wako nyuma ili wakue na baadaye wawe kampuni kubwa ambazo zinaweza hata kuuza nguo nje ya Tanzania. Hilo ndilo lengo letu,” amesema Erasto.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika biashara yanaweza kuwa chachu ya kuwafungulia vijana na wafanyabiashara fursa mpya, hasa katika kipindi ambacho ununuzi na uuzaji wa bidhaa kwa njia za kidijitali unaendelea kupata nafasi kubwa katika jamii.

Kwa hatua hiyo, ubunifu wa Erasto unaonyesha namna wanafunzi wa UDSM wanavyotumia ujuzi wa teknolojia kutengeneza suluhisho zinazolenga kutatua changamoto za kila siku, huku pia ukitoa fursa kwa sekta ya mavazi kuingia zaidi katika uchumi wa kidijitali.

Post a Comment

0 Comments

UDSM YABUNI MFUMO WA KUPIMA NGUO KABLA YA KUNUNUA