📍TPDC Yatajwa Nguzo Muhimu ya Dira ya Taifa ya Nishati Safi na Mazingira
Na Merina Makasi, DODOMA
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limetajwa kuwa miongoni mwa taasisi zinazotoa mchango mkubwa katika juhudi za Taifa za uhifadhi wa mazingira kupitia uendelezaji wa matumizi ya nishati safi ya gesi asilia, hatua inayosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira.
Pongezi hizo zimetolewa leo Juni 5, 2026 na Mkuu wa Tawi la Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.
Brigedia Jenerali Mabena amesema TPDC imeendelea kutekeleza kwa mafanikio jukumu lake la kugundua, kuchakata na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia nchini, jambo ambalo limeongeza upatikanaji wa nishati mbadala na rafiki kwa mazingira.
Ameeleza kuwa kwa miaka mingi dunia imekuwa ikitegemea zaidi matumizi ya dizeli na petroli katika shughuli za usafiri na uzalishaji viwandani, lakini matumizi ya gesi asilia yanafungua ukurasa mpya wa matumizi ya nishati safi inayochangia kupunguza uchafuzi wa mazingira.
“Nimejionea mfano wa gari linalotumia gesi asilia. Hii ni nishati safi ambayo siyo tu inalinda mazingira, bali pia ni nafuu na inaweza kumuduwa na wananchi wengi,” amesema.
Amefafanua kuwa tofauti na mafuta ya dizeli na petroli yanayozalisha hewa chafu inayochangia ongezeko la gesijoto na athari nyingine za kimazingira, gesi asilia hutoa kiwango kidogo cha uchafuzi na hivyo kuwa suluhisho muhimu katika kulinda mazingira na afya za wananchi.
Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabena, matumizi ya nishati safi yanaendana moja kwa moja na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuijenga Tanzania yenye maendeleo endelevu na mazingira salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele agenda ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi, hatua ambayo imeifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Nilipotembelea banda la TPDC nimejiridhisha kuwa ni miongoni mwa wadau wakubwa wanaochangia kwa vitendo kuhakikisha mazingira yetu yanabaki kuwa salama kupitia matumizi ya nishati safi,” amesema.
Sambamba na hilo, ameipongeza Wizara yenye dhamana ya mazingira pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kufanikisha tukio hilo lililohudhuriwa na Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Serikali.
Brigedia Jenerali Mabena ametoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira ili kufanikisha azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kijani ifikapo mwaka 2030 na 2050.
Ameongeza kuwa JKT nayo inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia mafunzo inayoyatoa kwa vijana katika kambi zake mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya kujenga kizazi chenye uelewa wa masuala ya mazingira na maendeleo endelevu.
Amesema kutokana na matarajio ya JKT kuwa na zaidi ya vijana 70,000 katika kambi zake kote nchini, matumizi ya nishati safi yatakuwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi mazingira wakati wa utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo maandalizi ya chakula na shughuli nyingine za kila siku.


0 Comments